Afrika Kusini imepongeza hatua ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ya kupunguza idadi ya majimbo nchini, moja ya matakwa makuu ya upinzani unaoongozwa na Riek Machar, kwa ajili ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
David Mabuza, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini ambaye pia ni mjumbe maalumu wa Sudan Kusini amesema kuwa, "hatua ya kimapinduzi iliyochukuliwa na Rais Salva Kiir imeandaa mazingira ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla ya kumalizika muda ulioanishwa unaomalizika ndani ya wiki moja."
Rais Salva Kiir amepunguza idadi ya majimbo ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kutoka 32 hadi 10. Akizungumzia uamuzi huo jana Jumamos, Kiir alisema "uamuzi tuliochukua ni wenye kuumiza lakini wa lazima iwapo utaleta amani."
Kiir aliongeza idadi ya majimbo ya nchi hiyo iliyojipatia uhuru wake 2011 kutoka 10 hadi 28 mwaka 2015 na kisha hadi 32 baadaye, wakati mgogoro na vita vya ndani nchini humo vilikuwa vimeshtadi.
Mwaka jana Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na Riek Machar, kiongozi wa waasi, walikubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu. Februari 22 ndio tarehe ya mwisho iliyoainishwa kwa ajili ya kuundwa serikali hiyo.
Umoja wa Afrika (AU) umeelezea kufurahishwa kwake na juhudi za kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Sudan Kusini ambao unalenga kurejesha amani katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko tangu kuasisiwa kwake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇