LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 2, 2020

RAIS MAGUFULI AOMBOLEZA VIFO VYA WATU 20 MOSHI NA ZAIDI YA 20 LINDI NA MIKOA MINGINE

IKULU, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli leo ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wakitoka katika Ibada huko Moshi mkoani Kilimanjaro, na kwa familia za watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha kutokana na madhara ya mvua kubwa zinazonyesha mkoani Lindi na mikoa mingine hapa nchini.

Watu 20 waliofariki dunia Mjini Moshi, walikuwa miongoni mwa watu waliokusanyika katika viwanja vya Majengo kuhudhuria Ibada iliyoongozwa na Boniface Mwamposa, na wamefariki dunia baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka katika lango moja waliloelekezwa kupita ili kukanyaga mafuta ya upako. Katika tukio hili watu 16 wamejeruhiwa.

Watu wengine zaidi ya 20 wamefariki dunia Mkoani Lindi na katika Mikoa mingine hapa nchini ambayo imekumbwa na madhara yatokanayo na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.

Mhe. Rais ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo, na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na Majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.

Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi na Wakuu wa Mikoa wengine ambao Mikoa yao imepatwa na madhara ya watu kupoteza maisha kutokana na madhara ya mvua, kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuchukua tahadhali katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha vinasimamia ipasavyo tahadhali za kiusalama.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages