Hivi karibuni jeshi na kamati za wananchi wa Yemen walitekeleza operesheni muhimu ya ‘al-Buniyan al-Marsus’ dhidi ya utawala wa Saudi Arabia.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, operesheni hiyo ya kijeshi ina umuhimu mno katika pande kadhaa.
Sababu ya kwanza ya umuhimu wa operesheni hiyo ni kujibu mapigo Wayamen dhidi ya mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia. Baada ya jeshi na kamati za wananchi kushambulia taasisi za shirika kubwa la mafuta la Saudia la ARAMCO Septemba mwaka jana na kutoa pigo kubwa kwa utawala waAl Saud, hamu ya pande mbili hususan Saudia na Ansarullah pamoja na waitifaki wake ya kufanya mazungumzo iliongezeka sana..
Licha ya kuwa, mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia yaliendelea, lakini kwa namna fulani kiwango cha mashambulio hayo kilipungua. Harakati ya Ansarullah na waitifaki wake pia, nao walichukua za kujizuia na kufanya juhudi za kuonyesha nia njema walionayo ya kuhakikisha kwamba, vita vya Yemen vinahitimishwa. Pamoja na hayo, kwa mara nyingine majuma mawili yaliyopita, kiwango cha mashambulio ya muungano vamizi wa Saudia Arabia kimeongezeka katika maeneo ya kaskazini mwa Yemen na eneo la Neham katika mji mkuu Sana’a limelengwa na mashambulio ya wavamizi hao.
Kwa msingi huo, jeshi na kamati za wananchi wa Yemen katika kujibu duru mpya ya mashambulio ya wavamizi, zimetekeleza operesheni iliyopewa jina la al-Buniyan al-Marsus ili kuthibitisha kwamba, zina uwezo wa kujibu mapigo dhidi ya mashambulio hayo ya Saudia na washirika wake.
Muhammad Abdul-Salam, msemaji rasmi wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, operesheni ya al-Buniyan al-Marsus imefanyika kwa shabaha ya kujibu hujuma na uvamizi wa utawala wa Aal Saud na waitifajki wake huko Neham.
Sababu ya pili ya umuhimu wa operesheni hiyo ni kuwa, kwa mara nyingine tena imedhihirika kuwa, taasisi za mafuta za Saudia zinadhurika mno na kwamba, Wayamen wana uwezo wa kuzishambulia taasisi hizo. Katika operesheni hiyo ya kijeshi, taasisi za mafuta za Saudia zilizoko Jizan zilishambuliwa na kusababisha hasara.
Sababu ya tatu ya umuhimu wa operesheni ya kijeshi ya al-Buniyan al-Marsusi ni kukombolewa kutoka mikononi mwa uvamizi wa Aal Saud eneo lenye ukubwa wa kilomita 2500. Eneo hilo la kistratijia linajumuisha miji ya Ma’rib, Sana’a na Jawf.
Ama sababu ya nne ya umuhimu wa operesheni ya al-Buniyan al-Marsus ni hii kwamba, katika operesheni hiyo kumedhihirika wazi udhaifu wa muungano vamizi wa Saudia katika rasilimali watu na wakati huo huo, operesheni hiyo imetoa pigo kubwa kwa muungano huo vamizi.
Brigedia Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza kuwa, maelfu ya askari wa maadui wameuawa, kujeruhiwa au kukamatwa mateka kufuatia operesheni hiyo. Kiwango hiki cha hasara ya rasilimali watu kinaripotiwa katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni akthari ya askari wa jeshi la Sudan waliokuwa wakipigana nchini Yemen chini ya muungano vamizi wa Saudi Arabia waliondoka katika medani ya vita.
Fauka ya hayo, kiwango hiki cha hasara kinaonyesha kuwa, mamluki wa Saudia hawana mafunzo ya kutosha ya kijeshi na hivyo hawana uwezo wa unaohitajika wa kupigana vita.
Na sababu ya tano na ya mwisho ya umuhimu wa operesheni ya al-Buniyan al-Marsus ni kupatikana ghanima na zana za kivita za muungano vamizi wa Saudi Arabia zilizoangukia mikononi mwa jeshi na kamati za wananchi wa Yemen. Zana hizo za kijeshi zinaweza kutumiwa kuendeleza vita dhidi ya utawala wa Aal Saud na waitifaki wake.
Kwa kuzingatia sababu hizo zilizotajwa mtandao wa habari wa al-A’hd umetangaza kuwa, operesheni ya al-Buniyan al-Marsus’ imethibitisha kwamba, jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen zinahesabiwa kuwa kizingiti na pigo la kistratijia dhidi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇