LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 1, 2020

KATIBU TAWALA MKOA WA SINGIDA DK. ANGELINA MAGENI, AANZA MWAKA 2020 NA SEKTA YA AFYA

Na John Mapepele, Singida
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dk. Angelina Mageni Lutambi amesema Serikali haitamfumbia macho mdau yoyote wa utoaji wa huduma za afya ambaye atafanya kazi   kwa mazoea bila kuzingatia  sheria na taratibu za utoaji huduma hizo na kwamba Serikali itakaa  na kujipanga  kwa pamoja ili kuwapatia wananchi huduma  bora wakati wote.

Dk. Lutambi amesema hayo wakati akifungua mkutano wa maandalizi ya mpango kabambe wa afya, ustawi wa jamii na lishe katika mkoa wa Singida  ambapo kwa  sasa  mkoa huu umekuwa na wadau wengi wanaotoa huduma za afya kutokana na Serikali kuweka mazingira wezeshi lakini  changamoto  kubwa ni  kuwa hakuna uelewa  wa pamoja  wa mdau gani anafanya nini katika eneo moja la utoaji wa  huduma za afya.

Amesema  Mkoa wa Singida  ni kitovu cha nchi ya Tanzania ambao watu kutoka  sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi hufika na kupita hivyo ni muhimu huduma inayotolewa katika mkoa huu kuwa katika kiwango cha kimataifa.

Aidha, amesema  mkoa wa Singida kuwa jirani na makao makuu ya nchi ni lazima uwe mkoa  wa mfano katika utoaji wa huduma za afya ambapo amemwagiza  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida kuboresha  huduma ili ifanane na hali halisi ya sasa.

Alisema  ili kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli  kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025 lazima  sekta ya afya iratibiwe vizuri  na wadau wote washirikiane na kupata namna ya utoaji wa huduma za afya ili wananchi waweze kupata afya bora.  

 “Ni kwa sababu hii ndiyo maana Serikali imeamua kuwakutanisha ili kujua namna bora ya kufanya shughuli hizo  kwa manufaa ya taifa” alisema Katibu Tawala.

Alisema baada ya mkutano huu kila mdau atafahamu  jinsi  bora  ya kufanya kazi baina yake  na mwingine ambapo  pia Serikali itatambua  na kupanga ushiriki mzuri baina ya Serikali na wadau wote wa afya katika Mkoa wa Singida.

Dk. Lutambi  alisisitiza kuwa mpango huo ni nyenzo inayotumiwa na timu ya uendeshaji wa  afya mkoani Singida katika kupanga, kutekeleza, kusimamia na kutathmini shughuli mbalimbali za afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Halmashauri zote  na vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya Jamii kila mwaka. 

Akizungumzia ya baadhi ya mafanikio ya mpango huo kwa mwaka 2019, Mratibu wa ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi  kwenye upande wa Afya Mkoa wa Singida, Dk. Abdallah Balla  alisema  kumekuwa na kuongeza kiwango cha wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka 86% (2018) hadi 99% (2019) kulingana na takwimu za NBS,kuongezeka kwa wateja wapya wa njia za kisasa za uzazi wa Mpango kutoka 27.4% (2018) hadi 32% (2019).

Dk. Balla alisema kumekuwa na kupungua kwenye kiwango cha udumavu kutoka 34% (2014) hadi 29% (2018) Kuongeza kiwango cha uchanjaji kutoka 106% (2018) hadi 117% (2019).

Aidha, upimaji wa virusi vya UKIMWI ngazi ya jamii, kwa mwaka 2019 jumla ya wananchi 35,973 walipimwa na kati yao wateja 602 (46%) ya wagonjwa wapya waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na kuunganishwa na vituo vya kutolea huduma.

Aliongeza kuwa huduma ya tohara kinga kwa wanaumie ilitolewa kwa wanaume 31008 sawa na 94% ya lengo la mwaka, ikihusisha Halmashauri zote za Mkoa wa Singida.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida Victorina Ludovick alimshukuru Dkt. Lutambi na kumhakikishia kuwa ataendelea kusimamia kikamilifu utolewaji wa huduma bora za afya  katika Mkoa wa Singida.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages