Shirika la Ujasusi la Marekani CIA limekiri kwamba siasa za vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran zimefeli na kwamba Tehran haipo tayari kufanya mazungumzo na Washington chini ya mashinikizo kwa mazingira yoyote yale.
Gazeti la New York Times limewanukuu viongozi wa ngazi za juu wa Marekani ndani ya shirika hilo katika moja ya uchambuzi wao wa hivi karibuni ambapo wamefikia natija hii kwamba, mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayajaweza kukaribisha mazungumzo kati ya Tehran na Washington. Likiashiria mipasuko iliyopo ndani ya muungano ulio dhidi ya Iran ambao ulianzishwa na Marekani, limeandika kuwa, licha ya Shirika la Ujasusi la CIA kufikia natija hiyo, lakini viongozi wa White House hadi sasa wameendelea kuunga mkono siasa zinazoitwa 'mashinikizo ya juu zaidi' dhidi ya Iran. Gazeti la New York Times limeongeza kuwa, katika uchunguzi wa shirika hilo la ujasusi la Marekani imebainika kuwa, kinyume na madai ya viongozi wa Washington, viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa wakikaribisha kupanuliwa uhusiano wao na nchi za eneo la Asia Magharibi.
Itakumbukwa kuwa mwezi Mei 2018 Rais Donald Trump wa Marekani alichukua hatua iliyo kinyume cha sheria na ya upande mmoja ya kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kwa jina la JCPOA ambapo sambamba na kuirejeshea Tehran vikwazo vikali, alitishia kuwa Iran ni lazima ifanya mazungumzo mapya na Washington. Katika kipindi hicho Washington na licha ya kutekeleza vikwazo vikali dhidi ya nchi hii, lakini haijaweza kufikia malengo yake ya kuifanya Iran iingie katika mazungumzo hayo chini ya mashinikizo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇