LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 9, 2020

ANGEL AKILIMALI: WANA-CCM MAJOHE EPUKENI TOFAUTI ZENU MKITEULIE CHAMA MGOMBEA BORA WAKATI WA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA HUU

Mjumbea wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuia ya Wanawake wa Tanzania (UWT) Taifa na Mkuu wa Idara ya Siasa na Habari ya vyombo vya Habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vinavyosimamiwa na Kampuni ya Uhuru Media (UMG), Angel Akilimali, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Majohe, Wilaya Ilala mkoa wa Dar es Salaam, akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Kata hiyo uliofanyika jana. Katikati ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata hiyo Nuru Mizumo na kulia ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata hiyo Selemani Mbinga. KWA PICHA NYINGI ZA MKUTANO HUO, TAFADHALI>> BOFYA HAPA


NA BASHIR NKOROMO, Majohe DSM
Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuhakikisha wanapitisha wagombea bora katika nafasi mbalimbali za uongozi, uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakapowadia, kwa kuwa mgombea watakayemteua akishateuliwa na Chama itakuwa ni lazima wana-CCM wote kumuunga mkono.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Angel Akilimali wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Kata ya Majohe, Wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa CCM wa kata hiyo uliofanyika jana.

"Ni lazima viongozi na wanachama kwa jumla wa CCM kuondoa tofauti zenu, na kuhakikisha mnateua mgombea bora kwa sifa siyo kwa undugu, urafiki, kujuana au kwa rushwa, kwa sababu mkiteua asiyefaa kwa sifa hilo linakuwa ni kosa lenu na vikao vya ngazi ya juu vya chama vikishampitisha itakuwa ni lazima kwenu kumuunga mkono ili Chama kishinde", alisema Angel ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Siasa na Habari ya vyombo vya habari vya CCM vinavyosimamiwa na Kampuni ya Uhuru Media (UMG).

Angel, alisema, kama yupo au atatokea mwana CCM yeyote kuwa na kero yoyote inayoweza kuzaa tofauti baina yake na wenzake ni lazima achukue hatua za kuziwasilisha kero hizo kwa viongozi wa eneo lake ili waishughulikie kero hiyo na kuitatua badala ya kukaa nayo moyoni na kusubiri kufanya hujuma wakati wa uchaguzi.

"Mimi katika nafasi yangu ya Mjumbe wa NEC, nawaomba wale wote watakaokuwa na kero za kichama waje hata kwangu tuzizungumze ili hatmaye tusipatie ufumbuzi, maana lazima mjue kuwa kila mnaposababisha mivutano katika chama mnakiumiza chama na wanachama wengine wenye nia njema.

Mimi sasa hivi ni M-NEC ambaye kwa bahati nzuri sasa naishi katika kata hii, siwezi kukubali chama kifanye vibaya katika uchaguzi wakati nipo, kuanzia sasa nawaomba mjitazame upya, muache tofauti zenu kabisa tukijenge chama ili kiwe imara.

Kumbukeni lengo la kuviunganisha vyama vya TANU na Afro Shirazi lilikuwa ni kupata chama kimoja chenye umoja na mshikamano zaidi, sasa ili lengo hilo liwe endelevu ni lazima mshikamano huo ufanyike ndani ya viongozi na wanachama wa CCM wenyewe", alisema Angel.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu, Angel aliwataka Viongozi wa CCM katika kata hiyo kujitokeza kuwania nafasi kwa maelezo kwamba CCM imeshatoa ruhusa kwa kiongozi wa Chama kuomba uongozi kwenye uchaguzi wa  viongozi wa serikali ambapo awali ilikuwa hairuhusiwi.

"CCM imesharuhusu, hata ukiwa ni kiongozi wewe chukua fomu ya kuomba uongozi, kama utashinda basi utaachia nafasi uliyokuwa nayo na utaendelea na hiyo uliyoshinda", alifafanua.

Aliwataka wana CCM katika Kata hiyo ya Majohe, kuhakikisha katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu inaongoza na kuwa ya kwanza katika kata zote za wilaya ya Ilala kwa kupata kura nyingi za urais ili kutoka nafasi ya pili ambayo ilishika.

Katika hatua nyingine Angel aliahidi kuipa Kata hiyo Katiba mpya za CCM baada ya kuona kuwa waliyokuwa nayo ni ya zamani ambayo haina mabadiliko kadhaa ambayo chama kimeshayafanaya.


1 comment:

  1. Ni kweli mpasuko wowote ndani ya chama ni hatari sana na viongozi wana wajibu mkubwa sana kuwaunganisha viongozi na wanachama wakishindwa kufanya hivyo kila mmoja atakwenda kwa njia yake,kiujumla kazi kubwa imefanyika chini ya mwenyekiti Rais wetu ndg John P.magufuri

    ReplyDelete

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages