Na
Munir Shemweta, WANMM NJOMBE
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza Wakuu wote wa idara
za Ardhi katika Halmashauri za mkoa wa Njombe kuandikiwa barua za kujieleza kutokana
na kushindwa kusimamia uingizaji taarifa za viwanja kwenye mfumo wa
Kielektroniki wa ukusanyaji kodi ya serikali.
Aidha, alitoa miezi
mitatu kuanzia tarehe 11 Januari 2020 hadi April 12, mwaka huu kwa halmashauri
za mkoa wa Njombe kumpatia taarifa ya kuingizwa viwanja vyote vya wamiliki wa
ardhi kwenye mfumo wa kielektroniki katika mkoa huo.
Dkt Mabula alitoa agizo
hilo jana katika kikao chake na watendaji wa sekta ya ardhi wa halmashauri sita
za mkoa wa Njombe akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya
ardhi pamoja na kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC).
Wakuu wa idara ya ardhi
walioangukia mikono ya Dkt Mabula kuhusiana na kuandika barua za kujieleza ni
kutoka Halmashauri za Njombe Mji iliyoingiza viwanja 7,301, Makambako 5,712,
Njombe Wilaya 326, Wanging’ombe 375, Makete 2156 na Ludewa viwanja 3,793.
Uamuzi wa Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi unafuatia kuelezwa kupitia taarifa ya mkoa wa
Njombe pamoja na zile za halmashauri zote za mkoa huo kuwa, kuanzia kipindi cha
Julai hadi Desemba 2019 ni viwanja
19,645 tu ndivyo vilivyoingizwa kwenye mfumo kati ya viwanja 40,961.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula,
utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki ulianza mwaka 2017
lakini cha kushangaza hadi kufikia sasa hakuna jitihada za dhati zilizofanywa
na baadhi ya halmashauri kuhakikisha viwanja vyote vinaingizwa kwenye mfumo huo
ili kurahisisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia pango la ardhi.
Alisema, kuingiza viwanja
kwenye mfumo wa kielektroniki siyo tu unarahisisha kutambua wamiliki wote wa
ardhi bali unasaidia kuwafuatilia wamiliki wanaokwepa kilipa kodi ya ardhi jambo
alilolieleza lisiposimamiwa kwa umakini litapunguza wigo wa ukusanyaji maduhuli
ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
‘’Uingizaji viwanja kwenye
mfumo wa kielektroniki ulianza tangu mwaka 2017 lakini bado hakuna
kilichofanyika hatuwezi kulea uozo huu unaoweza kuwapa mzigo wateja kutokana na
malimbikizo ya kodi’’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri Mabula
alisema, wizara yake inataka kuwa na malengo yanayoendana na kasi ya serikali
ya awamu ya tano na kuiagiza ofisi ya Ardhi ya Kanda kupitia takwimu za viwanja
vilivyo katika mfumo kwa halmashauri za mkoa wa Mbeya na kusisitiza haiwezekani
kuwa na Afisa Ardhi Mteule ama Mkuu wa idara ya Ardhi asiyefuatilia na kusisitiza
katika suala hilo wizara yake haitakuwa na msamaha.
Akigeukia ukusanyaji mapato
yatokanayo na kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alionesha kutoridhishwa na
makusanyo ya kodi hiyo kwa halmashauri za mkoa wa Njombe ambapo kufikia Desema
2019 halmashauri zote zilikusanya jumla ya shilingi 369,863,643.34 kiasi
alichokieleza kiko chini ya asilimia 50 ya makusanyo ya kodi ya ardhi katika
mkoa huo uliokuwa na lengo la Bilioni 1.2.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo
la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe unaotekelezwa na Shirika la Nyumba
la Taifa kwa gharama ya takriban bilioni 2.7.
Dkt Mabula mbali na
kuridhishwa na ujenzi wa jengo hilo amelitaka shirika la Nyumba la Taifa
kuhakikisha jengo hilo linakamilika mapema iwezekanavyo kwa kuwa lilichelewa
kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇