Tanzania na India zimeahidi kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia pamoja na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa na maendeleo endelevu baina ya nchi hizo mbili.
Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 71 ya Jamhuri ya India, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kuwa Tanzania na India ni ndugu na nchi hizo zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya diplomasia ya uchumi baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.
"Nchi ya Tanzania na India zina uhusiano mzuri, imara na wa muda mrefu ulianzishwa na baba wa Taifa Mwl. Julias Nyerere pamoja na Mahatma Gandhi. Na uhusiano huu umekuwa ukisaidia kuimarisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa" alisema Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa "sisi Tanzania na India ni ndugu, kwa hiyo basi tunawatakia sana kila la kheri katika kuiletea India maendeleo…lakini pia tukumbuke kuwa maendeleo ya India ni maendeleo ya Tanzania pia,"
Kwa sasa uchumi wa India na Tanzania umezidi kukuwa na kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya mataifa hayo. India imekuwa msharika mzuri wa maendeleo nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, maji, afya, teknolojia na elimu. Msaada wa India katika sekta ya maji hadi sasa, imeweza kusaidia kusambaza maji safi na salama katika kwa jiji la Dar es Salaam pamoja na upanuzi na uboreshaji wa mitambo ya maji Zanzibar.
Aidha, kwa upande wa sekta ya elimu, Tanzania na India zimeshasaini makubaliano ya kushirikiana kujenga kituo cha ufundi na pia msaada wa kuendeleza vyuo vikuu vya Zanzibar ambavyo vinatoa ujuzi unaolengwa kuwaendeleza wanawake walio na elimu ndogo au isiyo rasmi.
Kwa upande wake, Balozi wa India chini Tanzania, Mhe. Balozi Shri Sanjiv Kohli ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa India na kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa Tanzania na Taifa la India.
"Napenda kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya maendeleo baina ya mataifa haya mawili…..tukumbuke kuwa umoja ni nguvu na dhamira yetu ni kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu ni kuishi kwa amani umoja na mshikamano ili kukuza uchumi wetu," Alisema Balozi Kohli
Aidha, Balozi Kohli amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya kipekee kwa taifa la India kutokana na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa nchi ya India kijamii, kisiasa na kiuchumi.
"India inajivunia kuwa na uhusiano na mzuri na Tanzania ambao umewezesha mataifa haya kufanya biashara, uwekezaji, kujenga uwezo, ujenzi wa miundiombinu pamoja na maendeleo ya kiuchumi," ameongeza Balozi Kohli.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇