Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe akimpongeza Haitham bin Tariq Al Said kuteuliwa kuwa Sultan mpya wa Oman na akasema anataraji kuwa uhusiano wa Tehran na Muscat utaimarika pakubwa katika nyanja zote.
Rais Hassan Rouhani leo Jumatatu amemtumia jumbe wa pongezi Haitham bin Tariq Al Said Sultan Mpya wa Oman na kueleza kuwa uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman uliasisiwa kwa mujibu wa kuaminiana pande mbili wakati wa utawala wa mwendazake Qaboos bin Said Sultan wa Oman. Rais Rouhani ametoa mkono wa pole kwa Sultan wa Oman na wananchi wa nchi hiyo kufuatia kuaga dunia Qaboos bin Said na kusisitiza kuwa Sultan Qaboos alikuwa na nafasi athirifu katika kurejesha amani na uthabiti katika eneo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha namna marehemu Sultan Qaboos katika miongo mitano ya utawala wake alivyotekeleza hatua nyingi za kuwaletea ustawi na maendeleo wananchi na nchi yake na kuongeza kuwa Qaboos bin Said chini ya kuaminiana nchi mbili za Iran na Oman aliimarisha uhusiano wa nchi mbili hizi kwa misingi ya urafiki na udugu; na kudhihirisha kigezo cha uhusiano mwema kati ya nchi jirani.
Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia leo Jumatatu ameelekea katika ubalozi wa Oman hapa Tehran na kusaini daftari la maombolezo ya marehemu Sultan wa Oman.
Shirika rasmi la habari la Oman juzi alfajiri lilitangaza kuaga dunia Sultan Qaboos bin Said wa Oman akiwa na umri wa miaka 79. Haitham bin Tariq Sultan mpya wa Oman aliye na umri wa miaka 65 kabla ya kuchukua wadhifa huu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kama Waziri wa Mirathi na Utamaduni wa nchi hiyo na Mkuu wa Kamati ya Uchumi kwa jina la The Future Vision of Oman 2040.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇