LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 23, 2020

RAIS DK. MAGUFULI AMEMTEUA SIMBACHAWENE MAMBO YA NDANI BADALA YA KANGI LUGOLA, ZUNGU ABEBA MIKOBA YA SIMBACHAWENE

Rais Dk. John Magufuli amemteua George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuchukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa huku Rais akimteua Mbunge wa Ilala Musa Azan Zungu kuwa Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano na mazingira kujaza nafasi iliyoachwa na Simbachawene.

Taarifa ya Ikulu imesema,tarehe ya kuapishwa kwa Mawaziri walioteuliwa itatangazwa baadaye.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Mabalozi watatu watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kufuatia Mabalozi walikuwa katika nchi hizo kumaliza muda wao.

Mabalozi walioteuliwa ni Meja Jen. Jacob Kingu ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kabla ya kujiuzulu jana tarehe 22 Januari, 2020), Dk. John Stephen Simbachawene aliyekuwa Ofisi ya Rais (Ikulu) na Phaustine Kasike ambaye alikuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

Vituo vya kazi vya Mabalozi hao vitatangazwa baadaye na nafasi za Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Kamishna Jenerali wa Magereza zitajazwa baadaye.

Aidha, Rais Magufuli amewaongeza muda wa miaka 2 Mabalozi saba waliokuwa wakiiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali baada ya muda wao kumalizika.

Mabalozi hao ni George Madafa (Balozi wa Tanzania nchini Italia), Lt. Jen (Mstaafu) Paul Ignace Mella (Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC), Job Masima (Balozi wa Tanzania nchini Israel),  na Dkt. Emmanuel John Nchimbi (Balozi wa Tanzania nchini Brazil).

Wengine ni Dkt. Asha-Rose Migiro (Balozi wa Tanzania nchini Uingereza), Mhe. Benedict Mashiba (Balozi wa Tanzania nchini Malawi) na Sylivester Mabumba (Balozi wa Tanzania nchini Comoro).

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye kuanzia leo tarehe 23 Januari, 2020.
Nafasi ya Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji itajazwa baadaye.

Rais Magufuli pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi haraka kuhusiana na mkataba uliosainiwa kati ya kampuni ya kutoka nje ya nchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao hauna tija kwa nchi. 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages