Unaweza kusema kwamba kwa namna moja au nyingine Zanzibar ulikuwa kama mji mkuu wa Oman.
Tamaduni nyingi za Oman na Zanzibar zinafanana, kuanzia kwenye upande wa lugha ya kiswahili, chakula, mavazi na mtindo wa majengo yao vilevile yanashahabiana.
Ikiwa leo Zanzibar inaadhimisha miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka katika utawala wa kikoloni, Vilevile kisiwa hicho kinaendelea kumuenzi Sultan Qaboos bin Said Al Said wa Oman, mtawala wa muda mrefu katika nchi za kiarabu ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 79.
Sultan aliyemng'oa madarakani baba yake katika mapinduzi ya amani kwa ushriikiano na Uingereza mwaka 1970 na kuiweka Oman katika mwanzo mpya wa maendeleo kwa kutumia utajiri wake wa mafuta.
Mfalme wa Oman Sultan Qaboos aaga dunia
Nimezungumza na baadhi ya watu kutoka Zanzibar nao wamenieleza kwa nini Sultan Qaboos wa Omani kwa Zanzibar ni mtu anayeenziwa:
Salum Mkubwa Abdullah, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam anayesomea masuala ya maendeleo shahada ya uzamifu anasema kuwa Oman ina mchango mkubwa kwa Zanzibar,
kupitia uongozi wa Sultan Qaboos, aliweza kuendeleza mahusiano mazuri zaidi na Zanzibar haswa kwenye sekta ya elimu.
Zanzibar iliweza kujengewa chuo cha afya ambacho kwa sasa ni sehemu ya chuo kikuu cha Zanzibar yaani SUZA. Kilichopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Wanafunzi wa Zanzibar wengi walipata fursa ya ufadhili kwenda kusoma Oman.
Vilevile Oman imekuwa mstari wa mbele kuendeleza sehemu za kihistoria ambazo zilikuwa ni miongoni mwa utamaduni wao enzi hizo za utawala wao Zanzibar.
Kama vile Beit al Ajaib ( house of wonders), Palace Musium, Mtoni Ruins, na nyingine nyingi.
Oman imeweza kutoa mafunzo mengi kwa wafanyakazi wa makumbusho wa Zanzibar na hata kushiriki katika kuandaa matamasha.
Salum amegusia pia upatikanaji wa ajira hususan ajira za majumbani kwa akina mama, ajira ambazo zimewasaidia kina mama na familia zao kwa kuwasomesha watoto wao, kujipatia sehemu za kuishi na mahitaji mengine.
Ingawaje kumekuwa na malalamiko ya changamoto kwa baadhi ya waomani kuwanyanyasa baadhi ya wafanyakazi hawa kwa kuwapiga, na kuwaumiza sehemu zao za mwili.
Oman imeweza kurahisisha usafiri wa ndege katika eneo hilo na hivyo kufanya , uchumi na utalii kukua
Hamis Said ambaye ni mkazi wa Zanzibar anasema kua watu wengi wa Zanzibar wamechanganyika na Oman, yeye mwenyewe akiwa miongoni mwao.
Anatamani kuwa hata kiongozi aliyemrithi kuendelea kuenzi uhusiano huu mzuru.
Lakini kikubwa kwake anaona kuwa kipindi cha utawala wa Sultan Qaboos, Oman imekuza utalii wa Zanzibar kwa kiwango kikubwa. Kuna ndege ya kila siku kutoka Zanzibar kwenda Oman na kurudi.
Jambo ambalo limewarahisishia wageni kufika kiurahisi kutoka mataifa ya mbali.
Na vilevile kuna ubalozi mdogo wa Oman, Zanzibar
Ally Saleh ambaye alikuwa mwandishi wa BBC zamani lakini pia mbunge kisiwani Zanzibar anasema kuwa kuna sababu mbili kuu kwa Wazanzibari kumkumbuka Sultani Qaboos kwanza kwa wema na hisani yake katika kukuza maendeleo ya kisiwa cha Zanzibar.
Na sababu ya pili ni kwa sababu raia wengi wa Oman ni jamaa au wana undugu wa karibu na wazanzibari hivyo msiba huo ni wao wote.
Na kutokana na uhusiano huo milango ya Oman kwa Zanzibar imekuwa wazi.
Vilevile Oman imechangia mambo mengi au miradi mingi ya kimaendeleo katika upande wa ufadhili wa elimu na uhifadhi wa historia.
Ally Saleh amehitimisha kuwa Oman na Zanzibar uhusiano wao utaendelea kuepo hata kama Sultan Qaboos ameenda kwa sababu ya undugu waliokuwa nao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇