Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram wameshambulia kijiji magharibi mwa Chad na kuwaua wanakijiji kadhaa na kuwateka nyara wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa, Nouki Charfadine mkuu wa mkoa wa Ziwa Chad na afisa mmoja wa ngazi za juu wa Jeshi la Chad ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, magaidi wa Boko Haram wamevamia kijiji cha Alom katika eneo la Ziwa Chad na kuua watu wasiopungua wanne na kuwateka nyara wanawake kadhaa.
Tarehe 17 Disemba pia, magaidi wa Boko Haram walishambulia vijiji vinavyopakana na Alom na kuwaua wavuvi 14 huku watu wengine 13 wakitoweka katika tukio hilo.
Magaidi wa Boko Haram wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Ziwa Chad ambalo linapakana na Niger na Cameroon.
Pamoja na kuwa nchi za eneo hilo zimeunda kikosi cha kieneo cha kukabiliana na Boko Haram lakini hazijaweza kupunguza hujuma za magaidi hao ambao chimbuko lao ni kaskazini mwa Nigeria.
Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.
Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇