Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Tawi la CCM Chuini, Mohammed Sheikh Kheir akifungua kikao za Baraza la Umoja wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kaskazini Unguja, leo. Picha zaidi BOFYA HAPA
Kaskazini Unguja
Wajumbe wa ujumbe wa Umoja wa Wazazi wa Chama cha mapinduzi (CCM) wametakiwa kuongeza juhudi katika vita dhidi ya udhalilishaji ili kupata jamii bora.
Akifungua kikao za Baraza la Umoja huo wilaya ya Kaskazini Unguja, Mjumbe wa kamati ya siasa ya tawi la CCM Chuini, Mohammed Sheikh Kheir (Pichani, aliyesimama) alisema kufanya hivyo kunaenda sambamba na majukumu ya jumuiya hiyo na malengo ya serikali.
Kheir ambae pia ni sheha wa shehia ya Chuini alisema ili kushinda vita dhidi ya udhalilishaji kuna haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa kila mmoja katika jamii.
Alisema iwapo jumuiya hiyo itajikita kutoa elimu kwa wanachama wake na jamii kwa ujumla kuna uwezekano wa kufanikiwa kuiepusha jamii hasa wanawake na watoto dhidi ya vitendo hivyo jambo ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
“Tutakaposhirikiana na kila mmoja akatekeleza wajibu wake, bila shaka tutashinda vita hii ambayo sio serikali tu bali hata chama inapigana ili kupata jamii iliyostarabika”, alieleza Kheir.
Akizungumzia swali la kukiimarisha chama, Mjumbe huyo aliwaomba wanachama wa jumuiya hiyo kuwa wabunifu ili kuwavutia watu wengi kujiunga na chama kwa lengo la kuongeza kasi ya ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
“Jumuiya ya wazazi ndio nguzo na muhimili wa chama, hivyo ni vyema kila mmoja wetu akachukua jukumu la kuongeza wananchama ambao wataingia katika daftari la kudumu la wapiga kura na kuhakikisha wanakipigia kura chama chetu”, alisema Mjumbe huyo.
Aidha aliwapongeza wanachama wa jumuiya hiyo kwa kutekeleza miongozo, katiba na kanuni za jumuiya na chama kwa vitendo jambo linaloonesha ukomavu wa viongozi na kuwaomba kuendelea na mwenendo huo.
Nae Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo ambae pia ni Mjumbe wa baraza hilo Ali Khamis Ali alieleza kuwa chama wilayani humo kimejijipanga vyema kuongeza idadi ya wananchama kwa kutekeleza ajadi zilizotolewa na wagombea na kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 – 2020.
“Pamoja na mbinu nyengine za kisiasa, utekelezaji wa ilani kwa zaidi ya asilimia 90 katika wilaya yetu ni moja ya vivutio vikubwa vinavyowavutia wananchi na wananchama wa vyama vyengine kujiunga na CCM lakini bado tunahakikisha idadi yetu inaongezeka ili kushinda uchaguzi”, alieleza Khamis.
Akitoa taarifa kuhusu kikao hicho, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wilayani humo Biubwa Jabir alieleza kuwa baraza hilo ni moja ya utekelezaji wa miongozo ya chama na kwamba pamoja na kazi nyengine za kawaida mada mbali mbali zitawasilishwa.
“Hiki ni kikao cha kikatiba ambacho nashukuru wajumbe watapokea taarifa za utekelezaji lakini pia kuna mada mbili za uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na udhalilishaji zimewasilishwa ili kujenga uelewa wa wajumbe juu ya mambo hayo”, alieleza Katibu huyo.
Kwa mujibu wa Katibu huyo kikao hicho ni cha pili kwa mwaka huu ambacho pia kitatathmini shughuli mbali mbali zilizotekejezwa na umoja huo katika mwaka huu ambacho pia kitaweka maazimio ya kutekelezwa katika mwaka ujao.
MZEE GEORGE.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇