Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limesema makumi ya wahajiri wamepoteza maisha baada ya boti yao kuzama karibu na pwani ya Mauritania, wakiwa safarini kuelekea Ulaya kutafuta maisha.
Laura Lungarotti, Mkuu wa IOM nchini Mauritania aliyasema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, mbali na wahajiri 58 kufa maji, wengine 83 walinusurika baada ya kuogolea hadi katika ufuo wa bahari baada ya boti hiyo dhaifu ya plastiki kupinduka.
Amesema aghalabu ya wahajiri walioaga dunia katika ajali hiyo ni wanawake na watoto wadogo. Afisa huyo wa IOM ameongeza kuwa, majeruhi wanatibiwa katika hospitali ya mji wa Nouadhibou, magharibi mwa nchi hiyo.
Boti hiyo ambayo ilikuwa imebeba wahajiri karibu 180 inaripotiwa kutokea Gambia mnamo Novemba 27 na kwamba aghalabu ya wahajiri hao walikuwa vijana walio na umri wa miaka 20 hadi 30.
Haya yanajiri siku chache baada ya wahajiri wengine 67 kuzama na kufa maji katika pwani ya Libya baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), katika mwaka uliopita wa 2018, zaidi ya wahajiri haramu elfu mbili walipoteza maisha katika Bahari ya Mediterania wakiwa katika safari hatarishi ya kuelekea Ulaya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇