Serikali ya Muafaka wa Kitaifa yenye makao makuu yake mjini Tripoli na inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa imelaani vikali mashambulizi hayo, ingawaje haijataja idadi ya wahanga wa hujuma hiyo.
Hata hivyo vikosi waitifaki wa serikali hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu, Fayez al-Sarraj jana Jumatatu vilisema kuwa, mashambulizi hayo mapya ya wapiganaji wa Haftar yameua watu 14, aghalabu yao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.
Wanamgambo wa kamanda huyo muasi walilenga kijiji cha Al-Sawani, kusini magharibi mwa Tripoli, siku chache baada ya kushambulia kwa mabomu pia mji wa Umm al-Aranib, yapata kilomita 765 kutoka Tripoli.
Wakaazi wa mji wa Umm al-Aranib jana Jumatatu walifanya maandamano huku wakichoma matairi na kufunga mabarabara, kulalamikia mashambulizi hayo ya wapiganaji wa Haftar.
Tarehe 4 Aprili mwaka huu Haftar anayeungwa mkono na Saudia, Marekani na waitifaki wao wa Magharibi wa Kiarabu aliwaamuru wapiganaji wake waushambulie mji mkuu Tripoli kwa shabaha ya kuudhibiti, hatua ambayo imelaaniwa na jamii ya kimataifa. Zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine wasiopungua 5,700 wamejeruhiwa katika hujuma hizo za wapiganaji wa Haftar.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇