LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 17, 2019

UFAFANUZI KUHUSU MALIPO YA FEDHA ZA MIKOPO YA ELIMU YA JUU


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwajulisha wanafunzi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao wanakutana na changamoto mbalimbali kuwasiliana na menejimenti za vyuo vyao ili changamoto hizo ziwasilishwe HESLB na kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Ufafanuzi huu unafuatia maoni na malalamiko yaliyotolewa na wanafunzi wa vyuo mbalimbali, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salaam (CKD) kuhusu malipo ya fedha za vitabu na viandikwa (books and stationery) na malipo ya chakula na malazi (meals and accommodation) kwa wanafunzi waliobadilisha kozi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB Prof. William A.L. Anangisye ametoa ufafanuzi huu leo (Jumatatu, Desemba 16, 2019) jijini Dar es salaam katika kikao cha pamoja kati yake, menejimenti ya HESLB, menejimenti ya CKD na wawakilishi wa viongozi wa wanafunzi wa CKD.

“Wanafunzi wote wa taasisi za elimu ya juu wanapokutana na changamoto wasisite kuziwasilisha kwa menejimenti za vyuo ambavyo vitaziwasilisha HESLB au kwa taasisi sahihi, hata nyie mlipaswa kuanzia kwetu na tungeyafanyia yote kazi badala ya kutoa maelekezo ya masaa 72,” amesema Prof. Anangisye ambaye pia ni Makamu Mkuu wa CKD.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru, Naibu Makamu Wakuu wa CKD, Prof. Killian Bernadetha (Utafiti), Prof. David Mfinanga (Utawala), wawakilishi wa serikali ya wanafunzi CKD na watendaji wengine wa CKD na HESLB.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema kwa sasa HESLB inakamilisha malipo ya fedha za wanafunzi waliobadilisha kozi ambayo imepokelewa na HESLB kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) mwishoni mwa wiki na fedha hizo zitawafikia wanafunzi ifikapo keshokutwa, Desemba 18 mwaka huu.

“Kuna kundi la wanafunzi waliobadilisha kozi wakiwa vyuoni na taarifa hizo zilikua hazijatufikia, tumezipokea mwishoni mwa wiki na tunakamilisha malipo ambayo yatawafikia siku mbili zijazo,” amesema Badru na kufafanua:

Kwa mujibu wa Badru, kundi jingine linahusu malipo ya vitabu na viandikwa, ambapo malipo ya awamu ya kwanza ya jumla ya TZS 13.3 bilioni yameshafanyika na awamu ya pili ya TZS 1.1 bilioni itawafikia wanafunzi ifikapo jumamosi ijayo, Desemba 21 mwaka huu kwa kuwa wataalamu wetu wanakamilisha uchambuzi,” amesema.

Kwa upande wao, viongozi wa wanafunzi walioongozwa na Hamis Mussa walishukuru kwa kupata fursa na kuwasilisha masuala yao na kupata ufafanuzi.

Hadi sasa, jumla ya wanafunzi 49,485 wa mwaka wa kwanza wameshapata mikopo yenye thamani ya TZS 169.4 bilioni na kuvuka lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 45,000. Kati yao, wanafunzi yatima waliopoteza mzazi au wazazi wote wawili ni 10,383, wenye ulemavu (397), waliofadhiliwa masomo ya sekondari (3,128) na wengine wahitaji 35,577. Aidha, wanafunzi 78,337 wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 272.1 bilioni.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages