Meli ya MV.Muongozo ikiwa imeegesha katika Bandari ya Kigoma
Sehemu ya kontena ambazo zipo katika Bandari ya Kigoma zikisubiri kusafirishwa kuelekea nchi jirani za Jamhuri ya Domekrasia ya Kongo na Burundi.
Shehena ya nondo zikiwa katika Bandari ya Kigoma zikisubiri kusafirishwa kwa meli kwenda nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Mmoja ya wakazi wa Kigoma akiwa amebeba Nanasi kwa ajili ya kuzipakia katika meli ya MV.Maragalasi iliyokuwa inatarajia kusafiri kwenda nchini ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kupitia usafiri wa meli ndani ya Ziwa Tanganyika.
Baadhi ya abiria wa meli ya MV.Malagarasi wakipakia mzigo kabla ya kuanza safari kuelekea Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Meli ya MV.Mongozo pamoja na boti za abiria zikiwa zimeegeshwa katika Bandari ya Kigoma iliyopo ndani ya Ziwa Tanganyika.
Meli ya MV.Liemba ambayo ni moja ya meli kongwe nchini iliyotengenezwa mwaka 1913 ikiwa imeegesha katika Bandari ya Kigoma.
Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama akizingumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu miradi 27 inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za bandari za ziwa hilo.
Percival Salama ambaye ni Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa na TPA kuboresha huduma za bandari ndani ya ziwa hilo ambapo amezungumzia uboreshaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kwa sasa ambapo Serikali imetenga mabilioni ya fedha kuifanikisha.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika ukiwa katika hatua za awali.Ujenzi huo ni moja ya mradi wa bandari wa kuboresha majengo ya ofisi za TPA Ziwa Tanganyika.
Muonekano wa chelezo iliyopo katika Bandari ya Kigoma iliyopo Ziwa Tanganyika.
Na Said Mwishehe, Michuzi Globu-Kigoma
MENEJA wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama amesema uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) kuboresha miundombinu ya Ziwa Tanganyika ni sahihi kwani ziwa hilo limebeba utajiri mkubwa na kilichobaki ni kutumia fursa hiyo kwa maendeleo ya kiuchumi.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa wakati TPA ikiendelea na uboreshaji wa miundombinu ya bandari Ziwa Tanganyika, ni vema ikafahamika kuwa njia pekee ya kufikia soko la dunia kwa nchi ya Congo DRC ni lazima ipitie Ziwa Tanganyika kwa kuvuka upande wa Tanzania ili uende aidha kwenye bandari ya Dar es Salaam au Tanga.
Akizngumza na waandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa uboreshaji wa miundombinu ya bandari katika maziwa makuu nchini, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama ameeleza kwa kina kuhusu bandari zilizopo katika ziwa hilo.
Amefafanua kuwa bandari za Ziwa Tanganyika zipo katika mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Rukwa kwa upande wa Tanzania lakini pia ziwa hilo limepakana na nchi nne kwa pamoja kwa maana ya Tanzania yenyewe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Burundi.
"Na kama unatafuta asilimia ya kila nchi kwenye Ziwa Tanganyika Tanzania ina asilimia 45, DRC 41, Burundi asilimia 8 na Zambia asilimia 6. Na Ziwa Tanganyika ndilo Ziwa la pili kwa kina kirefu duniani,lina wastani wa urefu wa kina cha mita 1,470, kwa hiyo ukizungumzia uimara wa biashara ya kuhudumia nchi hizi nne maana yake unazungumzia miaka mingi ijayo.
"Kwa hiyo ni sahihi na ni vema kabisa kwa Serikali za nchi hizi nne zinapofanya uwekezaji wa miundombinu ya bandari pamoja na vyombo vya usafirishaji ili kuhakikisha wananchi wa nchi hizo wanapata huduma. Lakini la pili ambalo nataka niliguse kwenye hili eneo ni kwamba Ziwa Tanganyika na mikoa inayopakana na Ziwa Tanganyika na nchi hizi tumelala kwenye utajiri wa kutupwa yaani tupo sisi Tanzania kwenye ukanda wenye utajiri wa kutupwa duniani sio tu katika Afrika,"amesema Salama.
Amesema unapoizungumzia Tanzania kama nchi tajiri kama ambavyo amekuwa akieleza Rais Dk.John Magufuli mara nyingi na wote sasa Watanzania wanajua kuwa nchi yetu ni tajiri na kilichobaki ni fikra kuitumia vizuri ili kutumia vizuri fursa ile ya utajiri tulikuwa nao kubadilisha maisha ya nchi yetu kiuchumi pamoja na wananchi wake.
"Lakini kuna nchi jirani ya DRC hii Kongo nchi ile utajiri wa madini tu takwimu zinasema ina utajiri unaofikia trilioni 24 dola za Marekani huo ni utajiri wa madini tu. Sasa nilikuwa napiga hesabu kuangalia utajiri ule wa dola wa trilioni 24 za DRC ni sawa na bajeti za trilioni 31 za Tanzania za miaka mingapi.
"Nikakuta utajiri ule wa trilioni 24 Dola za Marekani ni wa madini tu kwenye nchi ya Kongo ni sawasawa na bajeti za Shilingi trilioni 31 za Tanzania kwa miaka 1780 sasa Mungu akupe nini ukiwa umepakana na nchi tajiri namna ile ambayo dunia unaangalia namna gani itafaidika na utajiri ule.
"Na njia pekee ya kufikia soko la dunia maana yake lazima upite Tanganyika uvuke Tanzania uende aidha kwenye bandari ya Dar es Salaam au Tanga ili uweze kufikia kwenye soko la dunia. Kwa hiyo utaona kwa kifupi kilichobaki kwetu Watanzania ni kujenga miundombinu sahihi, kujenga taratibu nzuri, kuweka mazingira rafiki ya kibiashara ambayo yatawafanya dunia iende Kongo na Kongo iende duniani,"amesema.
Ameongeza kuwa " Na tukiangalia hata kwenye utendaji wa Bandari za Ziwa Tanganyika kuanzia mwaka wa fedha 2014/15, 16 mpaka 17/18 na 2018/19 utaona mtiririko wa shehena tulivyohudumia. Mwaka 2014/15, tumehudumia tani 100,000, mwaka 2015/16 tumehudumia 139,000, kwa hiyo kulikuwa na ukuaji wa asilimia 28".
Amesema kuwa mwaka 2016/17 wamehudumia tani chini kidogo ya mwaka 2015/16 ambapo walihudumia tani 137,000, hivyo walishuka kwa asilimia 1.14 lakini mwaka 2017/18 wamehudumia tani 196,0000 kwa hiyo ukuaji wake pale ulikwenda kwa kasi zaidi wa asilimia 30.02 na mwaka uliofuata mwaka wa 2018/19 wamehudmia tani 199,831 sawasawa na ukuaji wa asilimia 1.14 ukilinganisha na mwaka 2017/18.
"Kwa hiyo hapa utaona kuna ukuaji na hasa kwenye kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia ile 2016/17 mpaka kwenye 2018/19. Mwaka huu wa 2019/2020 tumejiwekea kuhudumia tani 210,000 sawa na ongezeko la asilimia 9 ukilinganisha na mwaka jana na kwenye mapato vilevile kwa sababu shehena unayohudumia ndio vilevile pia na ukuaji wa wa mapato.
"Mwaka 2014/15 tulikuwa na Sh.bilioni 2. 09 ya mapato, mwaka 2015/16 bilioni 2.667, mwaka 2016/17 Sh. bilioni 4. 14 kwa hiyo utaona kuna ukuaji wa mapato. Mwaka 2017/18 hapa tulipiga zaidi kwani tulikwenda mapato ya Sh. bilioni 5. 93 na mwaka uliofuata mwaka jana tumekwenda na mapato ya Sh.bilioni 4. 148 ambapo hiyo tulishuka kidogo na sababu kubwa tilirekebisha ulipaji wa tozo,"amesema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇