Hatimaye baada ya wiki kadhaa za vikao vya uchunguzi vya wazi na vya faragha, kamati ya intelijensia ya bunge la wawakilishi la Marekani imemtuhumu rasmi Rais Donald Trump kuwa alitumia vibaya madaraka yake kuhusiana na suala la Ukraine na kujaribu kuizuia kongresi kutekeleza majukumu yake.
Kamati hiyo ya intelijensia imewasilisha matokeo ya uchunguzi wake katika ripoti ya kurasa 200 iliyoiwasilisha kwa kamati ya masuala ya kisheria ya bunge la wawakilishi. Kamati hiyo pia ilianza kazi yake ya kufuatilia suala la kumsaili rais wa Marekani tangu Jumatano iliyopita. Wademocrat wanaodhibiti bunge la wawakilishi wanataraji kuwa uchunguzi wa kamati mbili za intelijensia na kisheria hatimaye utaandaa uwanja wa kusailiwa Donald Trump.
Trump anatuhumiwa kutumia vibaya mamlaka ya kiti cha urais kutokana na hatua yake ya kuiomba rushwa Ukraine na kuzuia kuipatia Kiev misaada ya kijeshi ya Marekani. Aidha anatuhumiwa kutumia njia ya vitisho na kuzuia mtoa ushahidi kuhudhuria kikao cha uchunguzi ndani ya kongresi; na kwa njia hiyo anatuhumiwa kuikwamisha kongresi kutekeleza majukumu yake ya kisheria. Wademocrat pia wanaamini kuwa moja ya tuhuma hizo mbili inatosha kumfungulia mashtaka rais huyo wa Marekani.
Adam Schiff Mkuu wa Kamati ya Intelijensia katika Bunge la Wawakilishi la Marekani amesema baada ya kutolewa ripoti hiyo kuwa: Uchunguzi huu umeweka wazi sababu zenye mashiko zinazoonyesha kuwa Trump ametumia vibaya madaraka.
Hii ni katika hali ambayo, Warepublican kwa upande wao wanaamini kuwa hakuna uthibitisho wowote wa kweli wa kuweza kuthibitisha mwenendo huo mbaya wa Trump mkabala na Ukraine.
Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani anasema: Wananchi wa Marekani wanaweza kusoma muhtawa wa mazungumzo ya simu kati ya Rais Trump na mwenzake wa Ukraine na wataona kuwa hakukuwepo na aina yoyote ya ulazimishaji katika suala hili.
Pamoja na hayo, haionekani kuwa kuendelea kukana Trump na Warepublican katika kadhia ya mazungumzo yake ya simu yaliyozusha makelele ya Julai 25 na mwenzake wa Ukraine kutabadili mtazamo wa wale wanaounga mkono kusailiwa na kuuzuliwa rais huyo wa Marekani. Matokeo ya aghalabu ya chunguzi za maoni zilizofanywa nchini humo hivi karibuni zinaonyesha kuwa karibu nusu ya wananchi wa Marekani wanatilia mkazo kusailiwa na kuuzuliwa Trump. Suala hili linapata umuhimu kwa msingi huu kwamba tuhuma zinazomkabili zitaharibu pakubwa nafasi yake katika uchaguzi wa rais mwakani huko Marekani iwapo atasalimika kung'olewa madarakani kwa kura nyingi za Warepublican ndani ya seneti ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa chunguzi za maoni, sambamba na kufanyika vikao vya uchunguzi katika bunge la wawakilishi; wapiga kura wanaositasita na wenye mitazamo huru wameweza kushawishika kuliko hata waungaji mkono wa vyama vya Republican na Democrat kwamba Trump amefanya makosa hayo na kuwa kuna udharura wa yeye kusailiwa na kuuzuliwa.
Kwa kuzingatia kuwa inatabiriwa kuwa kikao cha mahakama katika seneti cha kusikiliza tuhuma dhidi ya Trump kitafanyika sambamba na kuanza uchaguzi wa utangulizi wa rais wa Marekani wa mwaka 2020; inaonekana kuwa mjadala wa kumuuzulu Trump utabadilika na kuwa mijadala muhimu ya mchuano wa uchaguzi bila ya kujali matokeo yake ya mwisho. Ndio maana Warepublican wakawa wanawatuhumu mahasimu wao kutoka chama cha Democrat kuwa wanatumia kadhia ya mazungumzo ya simu baina ya Trump na Rais wa Ukraine kama wenzo wa kulipiza kisasi kushindwa kwao katika uchaguzi wa mwaka 2016 na kujaribu kuathiri matokeo ya uchaguzi wa 2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇