Maafisa saba wa polisi na daktari mmoja ni miongoni mwa watu 10 waliouawa na wapiganaji wa kundi al-Shabab baada ya shambulio lililotekelezwa dhidi ya basi moja la abiria katika kaunti ya Wajir.
Askari hao wamedaiwa kutoka katika kitengo cha Anti-stock huku utambulisho wa raia wengine wawili waliouawa ukiwa haujulikani.
Walioshuhudia waliiambia BBC kwamba wapiganaji kadhaa waliokuwa wamejihami walishambulia basi hilo lililokuwa likielekea Mandera na kuwalenga watu wasiotoka katika eneo hilo baada ya kuwatenga kutoka kwa abiria wengine.
Kisa hicho kinadaiwa kufanyika kati ya miji ya Wargadadud na Kutulo.
- Marekani inashinda vita dhidi ya al-Shabab Somalia?
- Mateka wa Al-Shabab walazimishwa kusilimu
- Uvamizi wa al-shabab: Wakaazi wawaokoa wenzao
Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Stephen Ngetich amethibitisha tukio hilo lakini hakuweza kutoa idadi kamili ya walioathiriwa.
Bwana Ngetich amesema kwamba kikosi cha maafisa maalum tayari kimetumwa katika eneo hilo.
''Naweza kuthibitisha kwamba kundi moja la watu waliojihami walishambulia basi ambalo lilikuwa linaelekea Mandera siku ya Ijumaa jioni ijapokuwa bado hatujapata habari kamili kuhusu idadi ya waliouawa'', alinukuliwa akizungumza na gazeti la Daily Nation.
Basi hilo la Madina linadaiwa kushambuliwa mwendo wa saa kumi na moja jioni.
Shambulio hilo linajiri mwezi mmoja baada ya wapiganaji wa al-Shabab kushambulia kituo cha polisi cha Wajir katika jaribio la kutaka kuwaachilia huru washukiwa wawili wa ugaidi ambao walikuwa wanazuiliwa katika kituo hicho.
Kundi la wapiganaji wa al-Shabab nchini Somalia ambalo limekuwa likitekeleza mashambulio hayo mara kwa mara katika eneo hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo likisema kuwa limewaua takriban watu 10.
Katika taarifa iliyochapishwa katika mojawapo ya tovuti zake, kundi hilo linasema limewalenga abiria wasiokuwa Waislamu katika basi hilo.
Kisa hiki kimetokea katika barabara ambayo takriban Wakenya 28 waliokuwa wakisubiri basi moja walishambuliwa na kuuawa miaka mitano iliyopita.
Barabara hiyo ipo karibu na mpaka wa Somalia.
Tutazidi kukupasha zaidi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇