LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 2, 2019

MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI SHINYANGA


Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba (mwenye nguo nyekundu) akitembelea Banda la AGPAHI kwenye Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani Desemba 1,2019. Katikati ni Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele (katikati) akimwelezea Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Talaba kuhusu shughuli zinazofanywa na shirika la AGPAHI ikiwemo kuhudumia watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog 

Shirika lisilo la kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI imeungana na serikali ya mkoa wa Shinyanga kuadhimisha Siku ya UKIMWI duniani Desemba 1,2019 kwa kutoa huduma mbalimbali zinazolenga kupunguza maambukizi mapya ya VVU.


Maadhimisho hayo kwa mkoa wa Shinyanga yamefanyika katika kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Talaba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack. 


AGPAHI imeshiriki katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani kwa kutoa elimu ya VVU na UKIMWI na maonesho ya shughuli zinazofanywa na AGPAHI ikiwemo ujasiriamali kwa vijana wanaolelewa na shirika hilo. 

Akizungumza kwa niaba ya wadau wanaoshirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dkt. Nkingwa Mabelele amesema wadau ikiwemo AGPAHI wanaendelea kushirikiana serikali ili kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanapungua.

“Tunaendelea kushirikiana na serikali bega kwa bega ili kufikia asilimia 90 ya huduma za VVU na UKIMWI (malengo ya 90-90-90)”,amesema Dkt. Mabelele.

“Tunataka asilimia 90 ya wananchi wote wanatambua afya zao,90% ya wanaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU wanaingia katika mpango wa matumizi sahihi na ufuasi mzuri wa dawa na 90% inayobaki ni wale wote wanaotumia dawa kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha chini cha VVU”,ameongeza Dkt. Mabelele. 

Amesema Tanzania bila UKIMWI inawezekana hivyo kuwaomba wadau na jamii kwa ujumla kushikamana na kushirikiana na serikali ili kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanapungua. 

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga Talaba amesema kutokana na utafiti uliofanyika hivi karibuni,kiwango cha maambukizi ya VVU mkoa wa Shinyanga  ni  asilimia 5.9 (THIS 2017) ambayo iko juu ya kiwango cha taifa cha sasa cha asilimia 4.7 (THIS 2017) hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuachana na tabia hatarishi zinazochangia kuwepo kwa maambukizi. 

Talaba amewahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kupima ili wajue afya zao huku akiwakumbusha wanaume kufanyiwa tohara ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya VVU sambamba na kuachana na mila potofu zinazochochea maambukizi mapya ya VVU. 

“Tuendelee kuchukua tahadhari kwani UKIMWI bado upo na hauna chanjo wala tiba, bali una kinga na dawa za kufubaza makali ya VVU. Kama umepata maambukizi tafadhali endelea kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU na zingatia lishe kwani kuwa na maambukizi ya VVU haimaanisi kuwa ndiyo mwisho wa maisha yako”,amesema Talaba. 

Mkuu huyo wa wilaya ametumia fursa hiyo kuyapongeza mashirika yanayoshirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na kuyaomba yaongeze nguvu zaidi ili kufikia malengo ya 90-90-90. 

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani mwaka 2019 ni ‘Jamii ni chachu ya mabadiliko tuungane kupunguza maambukizi mapya ya VVU’.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages