LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 2, 2019

KILIMANJARO STARS KUFUNGUA DIMBA NA ZANZIBAR HEROES KOMBE LA CHALLENGE UGANDA


Na Asha Said, DAR ES SALAAM
TANZANIA Bara itafungua dimba na ndugu zao, Zanzibar Jumapili kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inayotaraiwa kuanza Desemba 7 hadi 19 mjini Kampala nchini Uganda.
Baada ya kufungua dimba na Zanzibar Heroes, Kilimanjaro Stars, mabingwa wa 1975, 1994 na 2010 watarejea uwanjani Desemba 10 kumenyana na Kenya kabla ya kukamilisha mechi za Kundi C kwa kumenyana na Djibouti Desemba 12.
Zanzibar wao baada ya kupambana na Tanzania Bara Jumapili, watarejea uwanjani Desemba 10 kumenyana na Djibouti kabla ya kukamilisha mechi za kundi lao kwa kukipiga na Kenya Desemba 12.
Kundi A linaundwa na wenyeji, Uganda, Burundi, Ethiopia na Eritrea, wakati Kundi B linaundwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan, Sudan Kusini na Somalia. 

Timu mbili za juu kutoka kila kundi zitaingia Robo Fainali zikiungana na mbili nyingine zitakazomaliza na wastani mzuri katika nafasi ya tatu. 
CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara saba, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
Mara ya mwisho Tanzania Bara ilitwaa Kombe hilo mwaka 2010 mjini Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Jan Borge Poulsen.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages