SHIRIKA
lisilokuwa la kiserikali la MEDO limeendesha majadiliano na wadau wa
elimu katika Shule ya Msingi Mchanganyiko ya Ilongero Halmashauri ya
wilaya ya Singida kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili
walemavu wa akili.
Akizungumza
kwenye majadiliano hayo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya
walemavu Duniani ambayo hufanyika Disemba 3 kila mwaka, Mratibu wa
shirika hilo Idd Hashim alisema lengo la kukutana na wadau hao ni
kuhakikisha watoto wenye ulemavu wa akili kutokubaguliwa katika Jamii.
Alisema
jamii ni lazima itambue walemavu ni watu kama watu wengine na kwamba
ulemavu walionao hawakuhitaji bali unaweza kumpata mtu yeyote, hivyo
jamii iache kuwaficha watu hao badala yake wawapatie haki zote za msingi
ikiwemo elimu.
"Wadau
tuendelee kuelimisha jamii juu ya watoto wetu hawa tusiwafiche, na
tuendelee kuiomba serikali iboreshe miundombinu ya shule."alisema
Hashim.
Mwalimu
mkuu wa shule hiyo Sijaona Nkurukwa alisema shule hiyo imeanzishwa
mwaka 1951 huku elimu ya kitengo maalumu ikianzishwa mwaka 2015 ambapo
watoto wenye ulemavu wa akili ni 29 wavulana wakiwa 18 wasichana 11.
Diwani
wa kata ya Ilongero Mh:Issa Mwiru aliwasisitiza wananchi kulipa kodi
ili serikali iendelee kuboresha miundombinu ya shule hasa kwa upande wa
watoto wenye ulemavu wa akili, na kuwaomba viongozi na jamii kwa ujumla
kuwajibika ili kuwaibua wazazi wanaowaficha watoto wao wenye ulemavu
huko majumbani.
Alisema
kutokana na shule hiyo kupokea watoto katika maeneo mengi ya
Halmashauri hiyo, hivyo jamii nzima kushirikiana kwa pamoja ili
kuwaboreshea miundombinu ya kujifunzia watoto hao.
Aidha
wazazi na wadau kwa ujumla walisema kuna baadhi ya wazazi wenye watoto
wenye ulemavu huo wanashindwa kuwapeleka watoto wao shuleni kutokana na
shule kutokuwa na mabweni ambapo inamlazima mzazi kumpeleka na
kumrudisha nyumbani mtoto jambo ambalo ni gumu kwao hivyo serikali
ingewajengea watoto hao mabweni.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇