Na Mwandishi wetu.
MBUNGE wa Jimbo la Songwe, Philipo Mulugo ameanza kuufanyia maboresho Uwanja wa Michezo ili uwe na hadhi hata ya kuzialika Simba na Yanga kufanyia mazoezi.
Amesema kuwa wachezaji wa timu hizo wakienda jimboni humo,licha ya kufanyia mazoezi kwenye uwanja huo, lakini pia watapata fursa ya kujionea vivutio vya utalii likiwemo Ziwa Rukwa, ambapo wanaweza kuwaona viboko, Mamba pamoja na kujipatia kitoweo cha samaki.
Tutazialika timu hizo zinapokwenda Mbeya kucheza Ligi Kuu na timu za Tanzania Prisons na Mbeya City, lakini pia hata Prisons na Mbeya City tutaziomba ziwe zinakuja mara kwa mara kufanya mazoezi pamoja na kucheza timu za jimbo hilo.
Amesema kuwa uwanja huo uliopo Makao Makuu ya Wilaya Songwe, Mkwajuni unaboreshwa ili michezo mbalimbali iwe inafanyika hapo.Baadhi ya michezo iliyotajwa ni; Mpira wa miguu, pete, kikapu, wavu na riadha.Pia utatumika kwa mikutano na sherehe mbalimbali.
Mulugo, amesema uwanja utaboreshwa vizuri ili uwe wa kisasa, kwani wamepanga kupanda nyasi nzuri za kisasa, utakuwa na njia ya kukimbia wanariadha, jukwaa kuu lakini pia ameshaongea na Mkurugenzi wa Halmashauri, Fauzia Hamidu ili awatangazie wananchi wajenge vibanda vya biashara kuzunguka uwanja huo.
Amesema maboresho ya uwanja huo utagharimu takribani sh. milioni 22.6 alizochangia yeye kwa kushirikiana na wadau mbalimbali aliowaomba.
Amesema kuwa uwanja ukikamilika wanatarajia kumwalika Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakembe kwenda kuuzindua.
Amesema kuwa ameamua kujenga uwanja huo ili kukidhi kiu ya wanamichezo wa wilaya hiyo waliokuwa wakihangaika kutafuta maeneo ya kuchezea ambapo baadhi walikuwa wanaenda mbali Shule Sekondari ya Maweni na shule ya Msingi Kaloleni.
"Pia nimesukumbwa na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk.Bashiru aliyoitoa hivi karibuni akiwa ziarani Zanzibar kuwa viongozi tuwe tunafanya mambo yanayoacha alama kama hili la uwanja,"amesema Mulugo.
Aidha Mulugo, amesema uwanja ukikamilika utakabidhiwa kwa Halmashauri ya wilaya, Idara ya Michezo kwa ajili ya kuuhudumia na kuutunza.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇