Charles James, Michuzi TV
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Walimu nchini kuhakikisha wanaanzisha
mchakato wa kufanya mazoezi asubuhi kwa wanafunzi kabla ya kuingia
darasani ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza
Mhe
Waziri Mkuu pia ameziagiza Wizara za Kilimo, Michezo kushirikiana na
Wizara ya Afya katika mapambano ya kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza
kwa kikubwa yamekua yakichangia vifo vya watoto na vijana ambao ndio
nguvu kazi ya Taifa.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua Wiki ya Kuzuia na
Kudhibiti Magonjwa Yasioambukiza sambamba na Mpango wa Taifa wa Kuzuia
na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza yaliyoenda sambamba na siku ya
kisukari duniani.
Amewataka
wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza
ikiwa ni pamoja na kubadili tabia na mwenendo wao wa ulaji wa vyakula
kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda.
Amesema
kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na
pombe; kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu;
kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na
mafuta. “Tujipange kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na
uharibifu wa mazingira na tabianchi.”
Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki.
“Katika
eneo hili, niweke msisitizo kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na
Makamu wa Rais Mama Samia Suluh Hassan.
“Tuendelee
kuhamasisha kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja
ambavyo husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi. Tutumie vikundi
vya joggingvilivyopo kwenye kata na mitaa au vijiji vyetu ili kupata
mwendelezo wa jitihada zao," Amesema Mhe Majaliwa.
Ameziagiza
Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya
wazi katika kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi
pia watumie maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi.
“Kwa
upande wa wanafunzi kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe
wanakimbia mchaka mchaka ili waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo
litawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza," Amesema.
Amesema
magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio kwenye jamii na ulimwenguni
kote, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2016 zinaonesha
kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na
asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
“Taarifa
za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kuwa,
pamoja na changamoto hizo za kiafya, magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri
sana nyanja nyingine za maisha. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha
miaka 20, kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya
zitafikia Dola za Marekani trilioni 47.”
Kwa
upande mwingine Mhe Waziri Mkuu amewataka watanzania kushiriki
kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24
kwa kuchagua viongozi waadilifu na wazalendo huku akionya kuchukuliwa
hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani..
“Vikundi
vya ulinzi wa jadi au vya ulinzi binafsi au vya mashabiki wa vyama vya
siasa havitaruhusiwa kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni au
maeneo ya uchaguzi.”
Waziri
Mkuu amesema kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Polisi,
Mgambo wenye sare na Maafisa wanaosimamia ulinzi vitatumika kuhakikisha
kunakuwepo na utulivu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Awali,Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
amesema magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha magonjwa ambayo hayawezi
kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Ameyataja
magonjwa hayo kuwa ni pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari,
saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho,
kinywa, masikio, pua na koo. “Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka
duniani kote na kuathiri nyanja zote za kimaisha.”
Waziri
Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania
ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa
yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa
milioni 4.2 mwaka 2018, ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.
Kwa
upande wao, wadau wa masuala ya afya wameipongeza Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza kiwango
cha bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 31 hadi sh. bilioni 270.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇