Bi. Maria Mosi akionyesha uso wa furaha wakati mtoto
wake Gloria Raphael mwenye umri wa miaka mitatu kuanza kusikia sauti kwa mara
ya kwanza baada ya kuwashiwa kifaa cha usikivu alichopandikiziwa kwa ajili ya
kumsaidia kusikia
Mtoto Ethan Riziki
mwenye umri wa miaka saba akilia baada ya kusikia sauti kwa mara ya kwanza.
Mtaalam wa huduma ya
usikivu Muhimbili Bw. Mathayo Majogoro (kulia) akirekebisha sauti kifaa cha
usikivu kwa mtoto Uebert Kigala mwenye umri wa miaka saba na nusu.
Daktari
Bingwa wa Upasuaji Masikio, Pua na Koo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-
Mloganzila, Dkt. Godlove Mfuko (katikati) akizungumzia zoezi la
uwashwaji wa vifaa vya usikivu (Switch on) kwa watoto wawili
waliopandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear Implant) mwanzoni
mwa Oktoba mwaka huu, kushoto ni Dkt. Aveline Kahinga na kulia ni Dkt.
John Masago.
Mtaalam wa Sauti Bw. Fayaz Jaffer akielezea namna vifaa vya usikivu vinavyofanya kazi.
Watoto
wawili wawashiwa vifaa vya kusaidia kusikia
Watoto wawili ambao
wamewekewa vifaa vya kusaidia kusikia katika hospiali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila
leo wamewashiwa vifaa hivyo na kuweza kusikia sauti kwa mara ya kwanza tangu
wazaliwe.
Mbali na zoezi hilo, pia
mtoto Uebert Kigala amerekebishiwa sauti kifaa alichopandikiziwa kwa ajili ya
kumsaidia kusikia ikiwa ni mwendelezo wa wataalam kufuatilia maendeleo yake ili
kuhakikisha kifaa kinafanya kazi kwa ufanisi.
Akizungumza na waandishi
wa habari Daktari Bingwa wa Upasuaji Masikio, Pua na Koo Godlove Mfuko, amesema
mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu Hospitali ya Mloganzila ilifanya upasuaji kwa
watoto watatu ambapo leo wawili wamewashiwa vifaa vyao ili waweze kusikia sauti.
“Hawa watoto hawajawahi kusikia
sauti tangu wazaliwe hivyo leo wataanza kusikia sauti mbalimbali katika
mazingira yanayowazunguka baada ya kuunganisha vifaa hivi na kuviwasha’’
amefafanua Dkt. Mfuko.
Sambamba na hilo, Dkt.
Mfuko ametoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kupima afya zao kwa sababu
asilimia 20 ya watu wenye tatizo la usikivu ndio wanaokuja hospitali huku
asilimia 80 wakibaki nyumbani.
Tangu kuanzishwa kwa huduma hii Juni 2017 katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili, jumla ya watoto 34 wamewekewa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear
Implants) hivyo kufanyika kwa huduma hizi nchini ni mwendelezo wa kuunga mkono
jitihada za Mh. Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Joseph Pombe Magufuli za
kuhakikisha wananchi wanafikiwa kwa urahisi.
Hadi sasa uwezo wa watalaam wazalendo kufanya upasuji umefikia asilimia
90 huku uwezo wa kuwasha vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implants)
watoto waliopandikizwa vifaa hivyo ambao walizaliwa wakiwa hawasikii
umeongezeka kufikia asilimia 100.
Gharama za upasuaji kwa mgonjwa au mtoto mmoja kuwekewa kifaa
cha kusaidia kusikia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni Tshs. 36 milioni
wakati akipelekwa nje ya nchi kwa matibabu hayo yanagharimu takribani Tshs. 80 hadi
Tshs. 100 milioni kwa mtoto mmoja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇