LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 13, 2019

WANAFUNZI WAJASIRIAMALI SHULE YA HOCET WASIITWE YATIMA- ASKOFU MWAMFUPE



Wanafunzi pamoja na baadhi ya wananchi wakicheza ngoma ya asili ya Maasai wakati wa sherehe za Mahafali ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Hocet, iliyopo Kata ya Shungubweni,wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani hivi karibuni. Kulia ni Mkurugenzi wa  na Mwasisi wa Hocet, Hezekiah Mwalugaja.



Mkurugenzi wa Taasisi ya Good For All (Washona Mahema), Askofu Edger Mwamfupe ambaye alikuwa mgeni rasmi, akijumuika pamoja na wanafunzi Angel Kiphutu na Tibet Eliya kukata keki wakati wa mahafali hayo.

Mkurugenzi wa Shule ya Sekondary Hocet, Hezekiah Mwalugaja akilishwa keki na mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne, Angel Kiphutu.



Mkurugenzi wa Taasisi ya Good For All (Washona Mahema), Askofu Edger Mwamfupe, akilishwa keki na mwanafunzi Tibeti Eliya.


Na Richard Mwaikenda, Mkuranga.

MKURUGENZI wa Taasisi ya Hope For All (Washona Mahema), Edger Mwamfupe ameupongeza uongozi wa Shule ya Sekondari ya Hocet, kwa kuwanusuru Watoto Yatima  kutoka kwenye hali ya mateso, kuwabadilisha tabia ya awali hadi kuwa na furaha ya maisha.

Kwa hatua nzuri waliyofikia, Mwamfupe aliutaka uongozi kuachana na mazoea ya wanafunzi hao kuwaita yatima au shule hiyo kuiita ya Yatima, bali iitwe ya shule maalumu kwa vile mambo mengi waliyofundishwa hapo yakiwemo ya ujasiriamali yameyatoa kwenye uyatima.

Mwamfupe ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akihutubia katika sherehe za mahafali ya Kidato cha Nne ya shule hiyo iliyopo wilayani Mkuranga,  Mkoa wa Pwani.

“Nawasihi kuanzia sasa muache kutumia jina Yatima, msiwarudishe watoto  kwenye unyonge, kwani mmefanya kazi kubwa ya kuwafundisha mambo mbalimbali ya kujitegemea, hawa sasa si sawa na watu wanaotegemea kila kitu kutoka kwa watu wengine. Hawa ni tofauti wana uwezo wa kujitegemea, Hivyo nashauri shule hii iitwe ya wanafunzi maalumu si Yatima tena,” alisema Mwamfupe, huku akipigiwa makofi.

Alitoa ushauri kwa uongozi kushirikiana na Taasisi yake kuweka mpango maalumu wa kuwawezesha  wahitimu kubaki shuleni hapo kwa kuendesha miradi ya ujasiriamali kwa kutumia elimu waliyopata badala ya kuwaachia kurudi mitaani walikotoka ambako ni rahisi kurudia tena katika hali waliyokuwa nayo awali ya maisha hatarishi..


Mkurugenzi wa shule hiyo, iliyoanzishwa  mwaka 2007, Mchungaji Hezekiah Mwalugaja, alisema kuwa wanafunzi wanaojiunga na shule ni yatima pamoja na wanaoishi kwenye mazingira magumu ambapo huwabadilisha tabia na mwenendo na hatimaye kuwa na tabia nzuri.

Alisema hufundishwa masomo ya kawaida, stadi za kazi, ujasiriamali, kilimo cha mbogamboga, matunda na mazao mbalimbali ambayo baadhi hutumika shuleni hapo kwa mahitaji ya chakula.

 Naye, Diwani wa Kata ya Shungubweni, Kamwiri Omari aliyekuwa mmoja wa wageni waalikwa katika mahafali hayo yaliyohudhuriwa pia na baadhi ya wananchi wa kata, alifurahia uwepo wa shule hiyo katika kata hiyo, ambapo aliahidi kutoa ushirikiano kutatua kero zinazoikabili.

Alisema kuwa tayari amewasiliana na Wizara ya Nishati ili umeme wa Rea ufike shuleni hapo na kwamba nguzo zinaletwa na umeme unaweza kuwashwa kabla ya Januari mwakani. Hivi sasa shule inatumia umeme wa  jua.

Pia, ameahidi kumpeleka shuleni hapo,Ofisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, akawapatie wahitimu 43 elimu ya mikopo kuunda vikundi ili wawezeshwe kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali.

Wahitimu Leila Mketo, Rahel Sarakikya na Fatuma Kalanje kila mmoja alikabidhiwa zawadi ya cherehani na kupata wasaa wa kuonesha kwa waalikwa nguo walizozishona.

Mahafali hayo yalihanikizwa kwa kwaya, ngoma za asili, shoo ya mitindo ya nguo na walioshinda michezo mbalimbali walizawadiwa ikiwemo mbuzi iliyotwaliwa na timu ya Shungubweni FC iliyoishinda timu ya Mamba FC. Zote kutoka kata hiyo ya Shungubweni.

Pia palifanyika michezo ya kuvuta kamba, kukimbia na yai likiwa kwenye kijiko mdomoni, kula apple zilizoning’inizwa kwenye kamba, Mr & Miss Hocet na mingineyo.








Mkurugenzi wa Taasisi ya Good For All (Washona Mahema), Askofu Edger Mwamfupe akihutubia katika mahafali hayo.

 Sehemu ya wageni waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
 Wanafunzi wanaoagwa wakiwa na furaha wakati wa mahafali hayo.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Askofu Mwamfupe akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi 43 waliomaliza kidato cha nne. Kushoto ni Mwalugaja.
.

 Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Askofu Mwamfupe akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi 43 waliomaliza kidato cha nne
Mkurugenzi wa Hocet, Mwalugaja akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi wahitimu


Wanafunzi wajasiriamali wakionesha mavazi waliyoyashona wakati wa mafunzo ya ushonaji shuleni hapo. Walikabidhiwa kila mmoja zawadi ya cherehani.Wanafunzi wajasiriamali Raila Mketo,Rahel Sarakikya na Fatuma Kalanje wakionesha


 Ni ngoma ya Kimasai
Wanafunzi wakitoa burudani ya shoo ya muziki.




Wanafunzi wakiwa wamejipanga baada ya kuonesha mitindo ya mavazi.


 Wahitimu wa Kidato cha Nne wakiwa katika picha ya pamoja.
 Askofu Mwamfupe akifurahia jambo na Outrich wa Hocet, Richard Solomonpamoja na Mdau wa Hocet, Joyce Massawe kwenye viwanja vya shule hiyo.


Wanafunzi wakishiriki mchezo wa kukimbia na yai kwenye kijiko.


Selina Lihanda akimkabidhi zawadi ya mbuzi Nahodha wa timu ya Small Stone iliyoishinda Mamba FC  katika mashindano yaliyoandaliwa na  uongozi wa shule ya Hocet katika Kata ya Shungubweni.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages