LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 12, 2019

UWEZO WA MAKOMBORA WA IRAN NGUVU ZA KIIATRATIJIA ZA KUZUIA MASHAMBULIZI YA ADUI

  • Kombora la Khorramshahr la Iran
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo hii imepiga hatua kubwa sana kieneo na kimataifa katika masuala ya ulinzi hasa upande wa nguvu za makombora.
Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran alisema hayo jana Jumatatu hapa Tehran mwanzoni mwa kongamano la taifa la utawala wa Kiislamu na huku akigusia mafanikio mbalimbali ya vikosi vya ulinzi vya Iran amesema: Leo hii Iran si tegemezi kwa nchi wala dola lolote kubwa, bali inajitegemea yenyewe kikamilifu. 

Uwezo wa Iran wa kumzuia adui hata asifikirie kuanzisha vita; kutokana na nguvu zake za makombora hadi kwenye vyuo na vituo vya kimkakati vya utafiti, umeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na jeshi imara ambalo hata maadui wanalazimika kukiri uwezo huo wa Iran. Marafiki wanafarijika na nguvu hizo, maadui wanaingiwa na kiwewe, na wachambuzi mbalimbali wanatenga wakati wao kuzizungumzia nguvu hizo.
Anthony Cordesman, mchambuzi wa kituo cha utafiti wa kiistratijia na cha kimataifa cha mjini Washington Marekani ametoa ripoti na sambamba na kukiri nguvu kubwa za kijeshi za Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi anasema:
Iwapo kutatokea chokochoko zozote zile za kijeshi dhidi ya Iran, Tehran itazusha tetemeko la mawimbi katika eneo hilo, kwani Iran ina mipango mingi ya kijeshi ya kulenga manufaa ya Marekani katika eneo hilo. 
Tathimini hiyo ni sehemu ndogo tu ya uhakika wa mambo kuhusu nguvu za kijeshi za Iran; nguvu ambazo kila kukicha zinazidi kuwatia kiwewe maadui. Maadui hao walikuwa wakiona kwamba pengine Iran ingeliogopeshwa na vitisho na vikwazo vyao na hivyo kusita kulinda haki zake na usalama wa eneo hili nyeti.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya miongozo yake muhimu aliyoitoa kwenye sherehe za kumaliza mafunzo wanachuo cha chuo kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain AS alisema, lengo la siasa hizo za Iran ni kumzuia adui hata asifikirie kuanzisha vita dhidi ya taifa hili la Kiislamu. Alisisitiza kwa kusema: 
Maadui wanapaswa kutambua kuwa, kama watafikiria kuanzisha vita dhidi ya Iran, watakumbwa na majibu makali sana. Wanaweza kuwa waanzishaji vita, lakini kamwe hawatokuwa watakaomaliza vita hivyo.

Wiki iliyopita pia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema katika moja ya miongozo yake wakati alipoonana na maelfu ya wanafunzi kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 13 Aban, Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistakbari wa Dunia kwamba:
Leo hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na hima ya vijana wa nchi hii, taifa la Iran lina nguvu kubwa za makombora yanayopiga shabaha kwa ustadi wa hali ya juu na kwa masafa ya kilomita elfu mbili...
Ukweli wa mambo ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa sana katika nguvu za makombora.
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema: Leo hii tumefanikiwa kuzalisha makombora ya kupiga vyombo vya baharini kutokea fukweni na kwamba makombora yote ya Iran kuanzia yale ya kilomita 200 hadi yale ya kilomita 2000 yanapiga shabaha kwa ustadi mkubwa sana. 
 Umuhimu wa nguvu hizo ni kumzuia adui hata asifikirie kuanzisha vita dhidi ya Iran. Tab'an Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuanzisha vita dhidi ya yeyote yule, lakini kama inapochokozwa kuwa inatoa majibu makali sana. Suala jingine ni kwamba, kuimarishwa nguvu za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo la dharura kutokana na madola ya kibeberu kujiimarisha mno kijeshi kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi na kuingilia waziwazi masuala ya eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuzilazimisha baadhi ya nchi kujilimbikizia silaha za madola hayo ya kiistikbari.
Kichekesho kikubwa ni kwamba Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazidi kujiimarisha kijeshi kwenye eneo hilo ambalo si lao, na wakati huo huo zinafanya njama za kila namna kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenye mpaka mrefu zaidi ya ufukweni katika Ghuba ya Uajemi, isijiimarishe kiulinzi na zinadai kuwa nguvu za kijeshi za Iran eti ni tishio kwa eneo hili. Lengo la maadui ni kutaka kuipokonya Iran uwezo wake wa kumzuia adui asianzishe vita dhidi yake. 
Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Amir Hatami alizungumzia jambo hilo jana Jumatatu akisema: Adui anamimina silaha nyingi kwenye eneo hili, ili kuipokonya Iran nguvu zake za kumzuia adui asishambulie. 
Hata hivyo nguvu za makombora za Iran hivi sasa ni moja na misingi mikuu ya uimara wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba taifa la Iran lina uwezo wa kutosha kabisa wa kukabiliana na chokochoko zote kwenye eneo hili. Iran imethibitisha kivitendo kwamba inatoa majibu makali kwa kitisho chochote kile dhidi yake.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages