Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli akipokea mfano wa hundi ya gawio yenye thamani ya Bilioni 169 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Prof. Ignatus Rubalatuka (wa pili kushoto) akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Deusdedit Kakoko Goodluck Shirima (kulia). Gawio hilo limekabidhiwa leo Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai na kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango. Picha zote na Othman Michuzi, Dodoma.
Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii - Dodoma
RAIS Dk. John Magufuli ametoa siku 60 kwa wakurugenzi na wenyeviti wa bodi za Mashirika, Taasisi na Kampuni za umma 187 kuhakikisa wanatoa gawio kwa Serikali, kinyume na hapo waondoke wenyewe katika nafasi zao kabla ya kuwachukulia hatua.
Amesisitiza ili kuhakikisha kampuni, mashirika na taasisi zinatoa gawio umefika wakati wa kuingia nao mikataba wote ambao wanapewa majukumu ya kusimamia kampuni hizo ili wakishindwa kuleta faida washitakiwe na ikiwezekana wafungwe kabisa, kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakidekezwa.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Novemba 24, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma baada ya kupokea gawio kutoka kwa mashirika, kampuni ya taasisi ambapo amesisitiza wote ambao hawajatoa gawio wahakikishe wanatoa ndani ya siku 60 ambazo ni sawa na miezi miwili kuanzia leo na watakaoshindwa watakuwa wamejifukuza kazi wenyewe.
"Serikali hadi sasa imewekeza mtaji wa Sh.Trilioni 59.6 kwa mashirika na taasisi 266 lakini pamoja na uwekezaji mkubwa kuna changamoto ya usimamizi na utendaji mbovu kwenye mashirika ambayo serikali ina hisa mapato yanayopatikana ni kidogo, Mfano mwaka 2014/15 Serikali ilikusanya Sh.bilioni 130 kutoka mashirika 24, 2015/16 zilikusanywa Sh.Bilioni 249.3 kutoka taasisi na mashirika 25,"amesema .
Hivyo Rais Magufuli amesema kutokana na hali hiyo Serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali ambazo zimeongeza ukusanyaji ambapo mwaka 2016/17 zilikusanywa Sh.Bilioni 677 kutoka taasisi 38,na mwaka 2017/18 zilikusanywa Sh.Bilioni 842.13 kutoka mashirika na taasisi 40, mwaka 2018/19 Sh.Trilioni 1.05 kutoka taasisi na mashirika 79.
Amefafanua ni vema tukajiuliza katika mashirika hayo 266 yaliyochangia 79 na Serikali imeweka mtaji wa Sh.Trilioni 59.6, yanabaki mashirika 187 ambayo hayana habari ya kuchangia wakati yana bodi, na bodi zina wenyeviti ambao wanalipana posho kila wanapokaa, wakurugenzi wanapanga semina, mikutano, wanasafiri, wanastarehe, wana magari na serikali imeweka pale fedha zake.
"Kuna mashirika ambayo mishahara yake inalipwa na Serikali na wengine wamepewa nyumba. Unaweza kujiuliza katika situation ya namna hiyo ungekuwa wewe ndo Rais ungefanyaje?Tena unaweza kukuta wengine wapo hotelini wanaangalia TV, fedha ambazo Serikali imewekeza katika mtaji huo ni za watanzania,"amesema.
Amesema waliopewa jukumu la kusimamia mashirika , kampuni na taasisi hizo kila siku wanafanya biashara lakini wakizungumza wanasema wanapata hasara lakini magari wanayo, mikutano wanafanya, wanakwenda katika starehe mbalimbali lakini gawio wameacha zinatolewa na kampuni 79.
Hivyo amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango kuwaandikia barua wanaosimamia mashirika hao ya kuwataka ndani ya siku hizo 60 wawe wametoa gawio kwa Serikali na kwamba muda wa kubembelezana umekwisha.
Amefafanua kuwa kama mwenyekiti ameteuliwa na yeye ni vema siku hiyo ikifika akajiondoa mwenyewe kwani hatakuwa mwenyekiti tena na kama ameteuliwa na mwingine pia wajiondoe wenyewe."Kama ni Mkurugenzi naye ajihesabu hayupo, wapo wanaolipwa mishahara Sh.Milioni 15 kwa mwezi, halafu hakuna gawio hata senti tano why?hufai kuwepo,"amesema.
Wakati huo huo Rais Magufuli amemwambia Dk.Mpango awaandike barua wale wote wasiokuwepo kwenye orodha ya mashirika 79 yaliyotoa gawio na orodha yao anayo. "Sasa hawa wengine wenye vibuli hivi ni wanani?Katibu Mkuu na Msajili baada ya siku 60 ambaye hataleta gawio lolote ajihesabu hayupo."
Hata hivyo amesema haijalishi Serikali ina hisa kiasi gani hata kama ni asilimia tano wanapaswa kutoa gawio na kwamba hakuna sababu ya kufanya biashara ya hovyo."Nchi za Scandinavia zinajiendesha kwasababu ya magawio zina watu waaminifu, hapa kwetu tunakila kitu bado tunashindwa kujisamamia na kwenda kuomba ufadhili kwa nchi hizo,"amesema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇