WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amempa siku tatu Kaimu Mweka Hazina wa wilaya ya
Itigi, Bw. Optatus Likiliwike ahakikishe anarejesha sh. milioni 1.6
ambazo alijilipa posho kinyume cha utaratibu.
“Kabla
sijamaliza ziara tarehe 7, nataka nione pay in slip kuthibitisha kuwa
fedha hiyo imerudishwa. Adhabu yako kaweke fedha benki, niione hiyo pay
in slip kabla sijaondoka," amesema Waziri Mkuu.
Ametoa
agizo hilo leo (Ijumaa, Oktoba 4, 2019) wakati akizungumza na watumishi
wa wilaya ya Manyoni ambao wanajumuisha Halmashauri za Wilaya za Itigi
na Manyoni.
"Wewe
si ndiye Otto au Optatus? Mwezi Julai ulilipwa posho ya safari ili
uende Dodoma kukamilisha mahesabu ya bajeti lakini hukwenda. Taratibu za
fedha zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?," alihoji
Waziri Mkuu.
“Nilichukua
fedha lakini kutokana na majukumu mengi niliyo nayo, sikwenda nikawa
naenda wikiendi na kuna kazi nyingine haikuwa ni lazima niwepo Dodoma,"
alijibu Bw. Likiliwike.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka afisa huyo arejeshe sh. milioni
196 za ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambazo zimetumika kinyume na
zilivyopangwa.
"Hizi
fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi. Hizi ni fedha za
retention, ni nani alikiuka maelekezo na kuamua kuzitumia kwa kazi
nyingine?" Waziri Mkuu alijibiwa kwamba ni Mkurugenzi na Mweka hazina
waliokuwepo kabla yake.
Waziri
Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Bw. John Mgalula
ambaye aliteuliwa wiki iliyopita asimamie marejesho ya posho za Bw.
Likiliwike pamoja na marejesho ya sh. milioni 196 ambazo mweka hazina
huyo ameahidi kuwa Halmashauri yake imetenga sh. milioni 70 ili
zirejeshwe kila mwaka.
Waziri
Mkuu amesema wanapaswa kutenga fedha zaidi ili fedha hiyo iweze
kurejeshwa haraka kwa Wakala wa Majengo nchini (TBA) ambaye ni
mkandarasi wa jengo la ofisi za Halmashauri hiyo.
Naye
Bw. Optatus Otto Likiliwike alisema kwamba fedha zinazodaiwa kutumika
zilikuwa zimetumwa na HAZINA kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini
zililazimika kuchotwa na uongozi uliopita ili zitumike kuweka
miundombinu ya kuanzisha Halmashauri mpya ya Itigi.
Alisema
waliohusika ukiukwaji huo ni Mkurugenzi aliyepita, Bw. Pius Luhende na
Mweka Hazina aliyepita Bw. Charles Mnamba. Hata hivyo, alikiri kwamba
fedha hizo hazikuombewa kibali cha matumizi hayo.
Akiweka
jiwe la msingi kwenye jengo hilo, Waziri Mkuu alisema anaweka jiwe hilo
kwa sababu ameridhishwa na maelezo ya Meneja wa TBA kuhusu ujenzi wa
jengo hilo.
Amewataka
madiwani wa Halmashauri hiyo wahoji matumizi ya fedha hizo na
wawaorodheshe wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo. “Kaeni
na mkaguzi wenu wa ndani, awape taarifa juu ya matumizi hayo,” alisema.
Pia
amewataka watumishi wa umma waheshimiane na watambue Mamlaka nyingine
kama za madiwani. Pia aliwataka wafuate taratibu na kanuni za utumishi
na siyo wajifanyie mambo kwa holela.
Awali,
Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,
Bw. Charles Fussi ahakikishe anarejesha mkopo wa sh. milioni 100 kutoka
benki ya CRDB ambazo walikopeshwa madiwani, wakarejesha kiasi lakini
Halmashuri haijazipeleka benki.
Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa deni hilo kutokana na malimbikizo ya muda mrefu na riba zinazotozwa na benki.
“Hakikisha
unamaliza hilo deni la sivyo hawa Waheshimiwa hawatapata stahili zao
hadi deni liishe. Pia unataka kusababisha mgogoro baina ya benki na
Halmashauri.”
Aliwataka
wadiwani hao waisimamie kwa karibu Halmashauri yao. “Madiwani
muiangalie Halmashauri yenu kwa kina. Hatuwezi kuendesha Halmashauri kwa
utaratibu huu wa kila mmoja kufanya kazi anavyotaka.”
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Itigi.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Watumishi wa Wilaya ya Manyoni,
mkoani Singida, kwenye ukumbi wa Halmashairi wilayani hapo, Oktoba
4.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇