Na Mwandishi Wetu, MOHA, Nkasi
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaondoa katika nyadhifa zao
viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa kwa
kushindwa kumudu majukumu yao baada ya kubaini kuwepo kwa wizi wa mara
kwa mara wa mifugo wilayani humo.
Lugola
pia ameagiza askari sita wa Kituo cha Polisi Namanyere na Kirando
wilayani humo waondolewe kutokana na wananchi wengi wanawalalamikia kwa
kushindwa kuwasaidia wanaporipoti matukio mbalimbali vituoni uwapuuza na
kuwakatisha tamaa.
Akizungumza
na wananchi katika Mkutano wa hadhara, mjini Namanyere, Wilayani humo,
Lugola alisema Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD), David Mtasya, Mkuu
wa Upelelezi wa Wilaya (OC CID), Emanuely Kajala na Mkuu wa Kituo cha
Polisi Namanyere (OCS) Wilayani humo, Ramadhani Msangi, lazima waondoke
katika Wilaya hiyo kwa kuwa wameshindwa kuimudu kazi yao ipasavyo.
“Wananchi
wa Namanyere, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa mkutanoni hapa na
wamelalamikia kama mlivyowasikia kutopata msaada kutoka kwa Jeshi la
Polisi pindi wanalipotoa mara kwa mara taarifa ya kuibiwa ng’ombe 278 za
wamiliki tofauti katika kituo cha polisi lakini hawasikilizwi,
wanazungushwa, wanapuuzwa mpaka kiasi kikubwa cha ng’ombe kimepotea,
licha ya kuwa wananchi 15 walioripoti polisi na mpaka sasa hawajapata
msaada wa polisi, hii haiwezekani na siwezi kukaa kimya, viongozi hawa
wameshindwa kazi, na lazima waondoke waje wengine,” alisema Lugola.
Aliongeza
kuwa, licha ya polisi hao kupokea malalamiko mengi vituoni, lakini
wanawaachia watuhumiwa hao wanaotuhumiwa kuiba ng’ombe za wananchi, na
pia uonekana mitaani kiasi kwamba wananchi hao wanapatwa na hasira na
kuanza kuichukia serikali.
Akitoa
kero yake kwa Waziri huyo, mkazi wa Namanyere, wilayani Nkasi, Felista
Mkomo, alisema mwaka jana aliibiwa ng’ombe wake lakini walifanikiwa
kuwakamata wawili ila wengine mpaka sasa hawajawapata, hata hivyo
aliripoti tukio hilo kituo cha polisi lakini mpaka sasa hakuna chochote
kilichofanyika na hakuna wezi aliyekamatwa.
“Mheshimiwa
Waziri mimi kero yangu ni wizi wa ng’ombe, niliibiwa mwaka jana, katika
kuwatafuta nikafanikiwa kuwapata wawili, lakini nikaamua kwenda polisi
kuripoti tukio hili la wizi, mpaka sasa hakuna taarifa zozote na
sijawapata ng’ombe wangu,” alisema Felista.
Aliongeza
kuwa Polisi hao wameshindwa kuwasaka mitaani watuhumiwa hao wa wizi,
kiasi kwamba wizi unaendelea wilayani humo na uwafanya kukosa mahali pa
kukimbilia kutoa malalamiko yao.
Waziri
Lugola akijibu kero hizo, alisema Serikali ya Dkt. Magufuli haiwezi
kuchezewa na mtu yeyote, na kamwe haiwezi kuona wananchi wake wanateseka
kiasi hicho, viongozi wa polisi wilaya wameshindwa kumudu kazi zao,
wameshindwa kuwahudumia wananchi, hivyo polisi hao wanapaswa kuondoka
wilayani humo, na wataletwa wapya.
Aidha,
Waziri Lugola alilitaka Jeshi la Polisi mkoani humo, kuwasaka wazazi na
walezi ambao wanawatumikisha watoto wao kufanya kazi katika Ziwa
Tanganyika badala ya kuwapeleka shule na kuendelezea wimbi la umaskini
katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa Ziwa mkoani humo.
“Watoto
wanapaswa kwenda shule, ni haki yao, watoto wengi wapo mitaani
wakifanya kazi wakiwa na umri mdogo, nawaagiza polisi mfanye msako
mkali, nyumba kwa nyumba, kuwakamata wazazi ambao watoto wao wapo ziwani
wakipara samaki, muwakamate,” alisema Lugola.
Waziri
Lugola amemaliza ziara yake Mkoani Rukwa, ambapo alitembelea Wilaya na
majimbo yote Mkoani humo, akisikiliza kero mbalimbali za wananchi pamoja
na kutembelea miradi mbalimbali ya taasisi zilizopo ndani ya Wizara
yake.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa
Kijiji cha Kirando, Wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa. Lugola amewaondoa
madarakani Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nkasi, Mkuu wa Kituo cha Polisi
Nkasi na Mkuu wa Mpelelezi wa Wilaya hiyo kwa kushindwa kumudu majukumu
yao baada ya kubaini kuwepo kwa wizi mifugo 278 wilayani humo. Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsalimia Mbunge wa
Jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy, wakati alipokuwa anawasili
ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimsikiliza Mkuu wa
Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, alipokuwa anampa taarifa ya ulinzi na
usalama ya Wilaya hiyo wakati wakielekea katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa unaotarajia kufanyika mwezi ujao nchini.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa
Kijiji cha Kirando, Wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa. Lugola amewaondoa
madarakani Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nkasi, Mkuu wa Kituo cha Polisi
Namanyere Nkasi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya hiyo kwa kushindwa kumudu
majukumu yao baada ya kubaini kuwepo kwa wizi mifugo 278 wilayani humo.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇