Mshambuliaji wa Timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars), Iddi Suleiman 'Nado' akichuana na Mchezaji wa Sudan katika Mchezo wakuwania kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN), uliopigwa katika dimba la El Merreikh Omdurman nchini Sudan, Stars imefuzu Michuano hiyo kwa faida ya bao la ugenini licha ya matokeo ya jumla ya 2-2.
Timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefuzu Michuano ya Mataifa Bingwa barani Afrika kwa Wachezaji wa Ndani maarufu kama CHAN baada yakuondoka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Sudan katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la El Merriekh Omdurman nchini Sudan
Taifa Stars inafuzu Fainali za Michuano hiyo itakayofanyika nchini Cameroon mwakani kwa faida ya bao la ugenini licha ya matokeo ya jumla ya bao 2-2.
Katika mchezo huo uliokuwa wa kasi zaidi kutokana na shinikizo la timu zote mbili, Stars ilitumia nafasi zake vizuri licha yakuruhusu bao la mapema dakika ya 30 ya mchezo lililofungwa na Mchezaji wa Sudan, Amr Suleiman.
Dakika ya 49 ya mchezo, bao safi lililotokana na faulo ya Erasto Nyoni liliirudisha Stars mchezoni pamoja na mabadiliko yaliyofanywa Benchi la Ufundi katika kipindi cha pili.
Mabadiliko hayo yalionekana kuzaa matunda zaidi kwa Kocha Etienne Ndayiragije kuingiza Washambuliaji na Viungo ilikutawala mchezo nakupata mabao ya ushindi. Wachezaji walioingia kuongeza nguvu kwa upande wa Stars, Mshambuliaji, Shaaban Iddi 'Chilunda', Ayoub Lyanga na Kiungo Salum Aboubakar 'Sure Boy'.
Benchi la Ufundi la Stars likiongozwa na Ndayiragije lilipata faida zaidi kupelekea kupata bao la pili dakika ya 78 lililofungwa na Mshambuliaji, Ditram Nchimbi.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Septemba 22, 2019 katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Taifa Stars ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwao, Sudan.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇