LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 8, 2019

Petroli, Mafuta ya Taa yachangia mfumuko wa bei wa Taifa kupungua


Charles James, Michuzi TV

MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioisha wa Septemba 2019 umepungua kwa asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioisha Agosti huku mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji ukiongezeka 

Akizungumza jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Bi Ruth Dawson amesema kupungua huko kwa mfumuko wa bei kunamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioisha Septemba mwaka huu imepungua.

Bi Ruth amesema mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi ulioishia Septemba 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti.

Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Septemba kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Septemba 2019 ukilinganisha na Septemba 2018.

" Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zimepungua bei kwa mwezi Septemba 2019 zikilinganishwa na bei za mwaka 2018 ni pamoja na mafuta ya taa kwa asilimia 1.0, Petroli kwa asilimia 3.3, Majiko ya Gesi kwa asilimia 1.5, Dawa za kuulia wadudu nyumbani kwa asilimia 2.2 na mafuta ya nywele kwa asilimia 1.3," Amesema Bi Ruth.

Amesema mfumuko wa bei za Taifa unapima kiwango na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Akizungumzia mfumuko wa bei kwa Nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia Septemba, 2019, Kenya mfumuko umepungua hadi asilimia 3.83 kutoka asilimia 5.00 huku Uganda ukipungua kutoka asilimia 2.1 hadi asilimia 1.9.
 Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Bi Ruth Dawson akitoa taarifa ya mfumuko wa bei ya Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages