Naibu
Kamishina (Operesheni) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Albert
Kingu akimkabidhi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ‘Road map’ na
makubaliano ya malengo waliyojiwekea Mamlaka hiyo na Mameneja wa Mikoa
katika kuhakikisha wanafikia malengo ya ukusanyaji mapato katika Mikoa
yao.
Kaimu
Meneja wa Mkoa wa Kodi wa Ilala, Bw. Steven Kuzeni akieleza taarifa ya
utekelezaji wa Ofisi yake kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu Kijaji alipotembelea Ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa kodi wa Ilala
na Kariakoo wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Ashatu Kijaji katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa kodi wa
Ilala, Jijini Dar es Salaam.
Katibu
wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Moses Dulle akifafanua jambo
wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na baadhi ya
Maafisa wa Ofisi za Mikoa ya Kodi ya Ilala na Kariakoo uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, akizungumza na
Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutoka Mkoa wa kodi wa
Ilala na Kariakoo alipotembelea ofisi hizo jijini Dar es Salaam
*******************************
Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameitaka Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), kuweka mifumo imara ambayo itamtambua kila
mfanyabiashara na bidhaa anayouza ili kuweza kukusanya kodi stahiki na
kupunguza mianya ya ukwepaji kodi.
Mhe.
Kijaji aliyasema hayo kwa viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wa Mikoa ya Kodi ya Ilala na Kariakoo, wakati wa ziara yake ya
kutembelea Ofisi za Mamlaka hiyo inayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Kijaji alisisitiza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ina jukumu kubwa la
kuhakikisha kwamba inavuka lengo la makusanyo iliyojiwekea ili kuweza
kumsaidia Mhe. Rais DKt. John Pombe Magufuli, atekeleze majukumu yake
kwa ufanisi na kulifikisha Taifa pale alipodhamiria.
“Naiagiza
Mamlaka kuanza zoezi la kukagua watumiaji wote wa mashine za utoaji
risiti za kieletroniki (EFD) hasa kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ili
kuhakikisha kila anayeuza anatoa risiti na anayenunua anadai risiti na
kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza makusanyo na kupelekea Taifa letu
kujiendesha kupitia fedha zetu wenyewe kwa kuwa hakuna Taifa huru bila
mapato’’ alisisitiza Dkt. Kijaji
Aliwataka
Maafisa wa TRA kutokaa ofisini badala yake wawatembelea wafanyabiashara
ili kuhakiki matumizi ya mashine za utoaji wa risiti za kieletroniki
(EFD).
Awali
Meneja wa Ofisi ya Mkoa wa Kodi wa Kariakoo, Bw. Alex Katundu
alimueleza Mhe. Kijaji kuwa Mkoa wake wa kikodi una jumla ya
wafanyabiashara waliosajiliwa na Mamlaka hiyo 22,279 na kati ya hao
wafanyabiashara 16,068 wanatumia mashine za EFD.
Alisema
Mkoa wa kodi wa Kariakoo kwa mwaka 2018/19 walidhamiria kukusanya
shilingi bilioni 138.66 lakini walifanikiwa kukusanya shilingi bilioni
109 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya malengo waliyojiwekea.
Katika
Mkoa wa kikodi wa Ilala, Kaimu Meneja Bw. Steven Kuzeni amesema katika
kuhakikisha Mkoa wake unakusanya ipasavyo kodi ya Majengo, wamedhamiria
kusajili majengo yote yanayozunguka Mkoa huo wa kikodi na hadi sasa
wameshasajili majengo katika kata 26 kati ya kata 32 zilizopo katika
eneo lake.
“Ofisi
yangu kwa mwaka 2019/20 ina mkakati kabambe wa kuhakikisha inaongeza
idadi ya walipa kodi ya mapato na wale wa ongezeko la thamani (VAT)”
Aliongeza Bw. Kuzeni.
Katika
hatua nyingine Kijaji amewapongeza watumishi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania kwa kuvuka lengo la makusanyo kwa mwezi Septemba ambapo
imekusanya sh. trilioni 1.76, kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa tangu
nchi ipate uhuru na kuwahimiza kukaa pamoja na Taasisi zote zinazofanya
kazi kwa karibu na Mamlaka hiyo ili kuona ni kipi kinaweza kuboreshwa
zaidi ili kuwapa fursa Watanzania kulipa kodi bila Serikali
kuwalazimisha.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇