Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
ASKARI Polisi sita na wafanyabiashara wawili wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mbalimbali likiwemo la kushawishi rushwa ya Sh. milioni 200 na kutakatishaji Sh.milioni 50.
Washitakiwa hao ambao wamefikishwa mahakamani hapo leo Septemba 30,mwaka 2019 wamesomewa mashitaka yao mbele ya mahakimu wawili tofauti ambao ni Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon mbele ya Hakimu Shaidi imewataja washtakiwa waliofikishwa hapo ni Sajenti Swedy Swedy (34), Koplo Mohamed (33), Koplo Jonas Lwezimula (38), wengine ni dereva Erick Kumburu (39) na mfanyabiashara Patrick Kumburu (40).
Imedaiwa, kati ya Julai 3 na 5 mwaka huu, maeneo ya Jamhuri na Indra Ghandi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, washitakiwa Kumburu, Erick, Lwezimula, Mohamed na Swedy walikula njama kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa Julai 3, mwaka huu katika maeneo hayo hayo, walipokea Sh milioni 48 kutoka kwa Aisha Gote kwa niaba ya dada yake Nazima Khambiye. Pia Julai 5, mwaka huu maeneo hayo, walipokea Sh milioni mbili kutoka kwa Khambiye kwa lengo la kutompeleka kito cha polisi.
Katika mashitaka la nne, inadaiwa kati ya Julai 3 na 5, mwaka huu kwa lengo la kudanganya, mshtakiwa Kumbuku alijifanya Ofisa wa Benki ya Tanzania (BOT) kitu ambacho alijua si kweli.
Aidha washtakiwa hao wanadaiwa wakiwa maeneo hayo, walijihusisha na muamala wa Sh milioni 50 huku wakijua kwamba fedha hizo ni zao la makosa tangulizi ya wizi na kulazimisha kupata fedha.
Hata hivyo, washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo na haina mamlaka ya kutoa dhamana.
Aidha, wapelelezi, kutoka jeshi la polisi Shaban Shillah, Emmanuel Njegele, Joyce Kitta na Ulimwengu Rashidi nao ambao wamefikishwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wakidaiwa kushawishi rushwa ya Sh milioni
Akisoma ya mashtaka, wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo amedai Desemba 17, 2018 huko Rainbow Social Club, Kinondoni, washtakiwa hao wakiwa maofisa wa uchunguzi, waliomba rushwa ya Sh milioni 200 kutoka kwa Diana Naivasha kama kishawishi cha kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.
Pia washitakiwa hao wanadaiwa, wakiwa waajiriwa wa Jeshi la Polisi, wakiwa katika Kituo cha Polisi Kawe walipokea rushwa ya Sh. milioni sita kutoka kwa Naivasha.
Alidai Desemba 18, mwaka 2018 washitakiwa hao walipokea rushwa ya Sh milioni sita kutoka kwa Naivasha na Desemba 19, 2018 washitakiwa hao wakiwa Kituo cha Polisi Kawe, walipokea Sh milioni mbili kutoka kwa Naivasha. Pia inadaiwa Desemba 23, 2018 washitakiwa walipokea rushwa ya Sh milioni mbili huku Januari 3, mwaka huu maeneo ya Tamarind Restaurant wilayani Kinondoni, walipokea rushwa ya Sh milioni mbili.
Aprili 13, mwaka huu maeneo ya Tripple 7 Bar and Restaurant, maofisa hao wa jeshi la polisi Idara ya Upelelezi inadaiwa walipokea rushwa ya Sh. milioni moja kutoka kwa Naivasha kama kishawishi cha kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.
Imeendelea kudaiwa kati ya Desemba 17,2018 na Aprili 13, mwaka huu maeneo yasiyojulikana jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Kitta alighushi maelezo ya Naivasha ya Desemba 17, 2018 ili kuonesha kuwa maelezo hayo ni ya kweli na yalisainiwa na Naivasha wakati si kweli.
Pia mshitakiwa Shillah na Njegele ambaye hakuwepo mahakamani, Aprili 13, mwaka huu wakiwa maeneo ya Triple 7 walikiuka amri halali ya kukamatwa na Mpelelezi wa Takukuru, Colman Lubis. Hata hivyo, washtakiwa wamekana mashitaka na upande wa mashitaka umedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Washtakiwa wameachiwa huru kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo Hakimu Rwizile aliwataka washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya taifa ambapo kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni 10.
Pia aliwataka kuwasilisha mahakamani hapo hati za kusafiria na mmoja kati ya wadhamini hao ametakiwa kuwa na hati au uthibitisho wa mali isiyohamishika. Mshitakiwa Shillah peke yake ametiza masharti na wengine walirudishwa rumande hadi Oktoba 16, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇