Na Ezekiel Mtonyole - Mtwara
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakayofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Manispaa ya Mtwara, Mkoani Mtwara.
Hayo yamesemwa leo mkoani hapa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi alipokuwa akitoa taarifa kuhusu Siku ya Wazee Duniani kwa niaba ya Wazriri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinisia, Wazee na watoto, Ummy Mwalimu.
Kamishna Ng’ondi amesema kuwa Chimbuko la Siku ya Kimataifa ya Wazee ni tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa kupitia azimio Na. 45/106 la Mwaka 1990 ambalo linazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisho siku ya Kimataifa Wazee kila ifikapo Oktoba Mosi ya kila Mwaka.
“Lengo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki na mahijaji ya wazee. Kwa msingi huu, kupitia siku hii jamii hupata fursa ya kutafakari mafanikio, fursa na changamoto ili kuendelea kuboresha hali ya maisha ya Wazee” alisema Kamishna Ng’ondi.
Ameongeza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani hutoa fursa kwa wazee wenyewe, Serikali, Jamii, Vyama vya Siasa, Madhehebu ya dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuungana, kushiriki, kutafakari, kubainisha na kutatua changamoto zinazowakabili wazee katika utekelezaji wa maazimio, mikataba na matamko mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa yanayowawezesha wazee kuleta maendeleo yao na jamii nzima. Ameitaja Kauli Mbiu kwa mwaka huu kuwa ni “Tuimarishe Usawa Kuelekea Maisha ya Uzeeni” ikiwa na lengo la kuhimiza nchi wanachama kuweka Mipango na mikakati ya kupunguza tofauti za watu katika jamii na kutoa fursa kwa makundi maalum kufaidika na fursa zilizopo na maendeleo yaliyofikiwa katika nchi husika.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Bi. Mwanaisha Moyo amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Mtwara watatoa huduma za afya na Ustawi wa Jamii kwa wazee na wananchi wote wakakojitokeza katika madhimisho ya Siku ya Wazee Duniani.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Mtwara Meja Mstaafu Mohamed Mbwana ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuwajali wazee katika huduma za Afya na msamaha wa kodi za majengo ya makazi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇