Waitifaki wawili wakubwa wa rais aliyeondolewa madarakani nchini Burkina Faso, Blaise Compaore, wamehukumiwa vifungo vya hadi miaka 20 jela kwa kupatikana na hatia ya kupanga mapinduzi ya mwaka 2015 dhidi ya serikali ya mpito nchini humo.
Mkuu wa zamani wa shirika la upelelezi la Burkina Faso, Jenerali Gilbert Diendere
amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kupatikana na hatia ya kufanya mauaji na kutishia usalama wa taifa.
Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso, Djibril Bassole ambaye analaumiwa kuwa ndiye aliyekuwa mratibu mkuu wa jaribio hilo, amehukumiwa kifungo cha miaka 10.
Mwaka 2015 Jenerali Gilbert Diendere ambaye alikuwa mkono wa kulia wa rais wa zamani wa Burkina Faso aliongoza kikosi cha Gadi ya Taifa na kuwashikilia mateka wajumbe wa serikali ya mpito, mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi mwaka uliofuata.
Jaribio hilo la mapinduzi lililoendelea kwa kipindi cha wiki moja lilishindwa lakini watu 14 waliuawa na wengine zaidi ya 250 kujeruhiwa wakijaribu kukabiliana na kundi la wafanyamapinduzi.
Waburkina Faso waliokuwa wamekasirishwa na jaribio la rais wa zamani wa nchi hiyo, Blaise Compaore la kutaka kubadilisha katiba kwa shabaha ya kurefusha utawala wake wa miaka 27 walimlazimisha kuondoka madarakani na kukimbilia nchi jirani ya Ivory Coast mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇