Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelekea mjini Moscow, Russia kwa ajili ya kuonana na kuzungumza na waziri mwenzake wa nchi hiyo Sergey Lavrov kuhusu masuala muhimu wa pande mbili.
Sambamba na ziara ya Zarif mjini Moscow, ujumbe wa kisiasa na kiuchumi ukiongozwa na Sayyid Abbas Araqchi, Naibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa umeelekea nchini Ufaransa kwa ajili ya kufuatilia mapendekezo ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Ziara ya Zarif mjini Moscow ina umuhimu wa kipekee hasa kwa vile imefanyika baada ya waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran kufanya ziara ya kuzitembele nchi tatu za Ulaya na Asia wiki mbili zilizopita.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza baada ya kikao cha Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kwamba: Kama nchi za Ulaya hadi tarehe 5 Septemba zitakuwa hazijachukua hatua zinazotakiwa katika kutekeleza ahadi zao ndani ya mapatano ya JCPOA, basi Iran itatangaza kuanza kutekeleza awamu ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mapatano hayo.
Aidha alisema, kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa na kuwasilishwa tarehe 8 Mei 2019 katika barua ya Iran kwa nchi za Ulaya, Tehran lazima itaanza awamu ya tatu ya kupunguza utekelezaji wa ahadi zake ndani ya JCPOA kwa mujibu wa vifungu vya 26 na 36 vya mapatano. Hata hivyo hivi sasa mazungumzo ya kina yanafanyika kuhusu hatima ya makubaliano hayo na kadiri siku zinavyopita ndivyo mwanya wa baina ya kubakia JCPOA au kuachana na makubaliano hayo unavyozidi kuwa finyu.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, nchi mbili za Iran na Ufaransa zimetoa mapendekezo mbalimbali kuhusiana na JCPOA. Kwa mujibu wa Mahmoud Vaezi, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mapendekezo hayo yametolewa baada ya mazungumzo ya masaa matano baina ya marais wa Iran na Ufaransa.
Jumamosi usiku, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumza kwa simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kusisitiza kuwa, kama nchi za Ulaya zitashindwa kutekeleza kivitendo ahadi zao ndani ya JCPOA, basi Iran itaanza kutekeleza awamu ya tatu ya kupunguza ahadi zake kwenye makubaliano hayo ya nyuklia.
Rais Ruhani alisema kuwa, msimamo wa asili wa Iran ni kuyalinda mapatano hayo na daima imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha kuwa hayavunjiki lakini wakati huo huo akasisitiza kwamba: Iwapo pande zote husika zitatekeleza kikamilifu vipengee vya JCPOA basi jambo hilo litaweza kudhamini usalama wa safari huru za baharini katika maeneo yote likiwemo eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz na hayo ni katika malengo makuu ya Iran kwenye mazungumzo ya hivi sasa.
Ukweli ni kwamba kitendo cha Marekani cha kutoheshimu vipengee vya makubaliano hayo na kujitoa bila ya sababu yoyote katika JCPOA kimefanyika kwa shabaha ya kukwamisha ushirikiano wa Iran na nchi nyingine. Inasikitisha kuona kuwa, baada ya hatua hiyo ya Marekani, nchi nyingine za Ulaya nazo hadi hivi sasa hazijachukua hatua yoyote ya maana ya kutekeleza kivitendo ahadi zao.
Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pande zilizofikia makubaliano ya JCPOA zinapaswa kuheshimu kikamilifu yaliyomo ndani ya mapatano hayo. Mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha baina ya Iran na Ulaya unaojulikana kwa jina la INSTEX ungelikuwa ni utangulizi wa kutekeleza nchi za Ulaya ahadi zao, lakini nchi hizo zimeshindwa kuutekeleza huku Iran ikiwa imeheshimu na kutekeleza kikamilifu ahadi zake zote, muda wote huu.
Hivi sasa juhudi za kidiplomasia za Ufaransa za kuyalinda mapatano ya JCPOA kupitia mapendekezo yake maalumu zinaweza kwa namna fulani kuangaliwa kwa jicho zuri, lakini kwa kuzingatia uzoefu wa huko nyuma wa kushindwa nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao, hakupatikani imani ya kutosha juu ya mapendekezo hayo mapya ya Ufaransa. Tofauti na nchi za Ulaya, nchi nyingine zilizomo kwenye makubaliano ya JCPOA yaani China na Russia zinaendelea na uhusiano wao wa kibiashara na Iran kama kawaida na wala kujitoa Marekani kwenye mapatano hayo hakukuzizuia nchi hizo kuendelea na uhusiano wao mzuri na Iran.
Hivi sasa inabidi tusubiri na kuona juhudi mpya za kidiplomasia za huko Moscow, Paris na Vienna zitasaidia vipi katika kipindi hiki cha siku chache zilizobakia kabla ya kumalizika muda wa siku 60 uliotolewa na Iran wa kuhakikisha nchi za Ulaya zinatekeleza ahadi zao, vinginevyo Tehran itatangaza awamu ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake ndani ya JCPOA.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇