Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, amekosoa hatua za Marekani za kuibua mizozo eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati.)
Maria Zakharova aliyasema hayo jana ambapo ambamba na kukosoa hatua hasi za Marekani za kuanzisha muungano wa baharini katika Ghuba ya Uajemi amesema kuwa, muungano huo hautasaidia kupatikana uthabiti katika eneo hilo. Zakharova ametoa kauli hiyo kufuatia matamshi ya siku ya Alkhamisi ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyedai kwamba Washington inafuatilia njia ya utatuzi wa mzozo katika eneo kupitia njia za amani sambamba na kuanzisha muungano tajwa.
Katika uwanja huo, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sambamba na kukosoa vikali mpango wa Marekani wa kuunda muungano katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) amesema kuwa ubunifu wa kidiplomasia wa Tehran katika ngazi ya kimataifa na eneo kwa ajili ya kutatua mzozo uliopo kwa njia za amani, ndio njia bora. Inafaa kuashiria kuwa, katika wiki za hivi karibuni, Marekani imefanya njama kubwa zenye lengo la kuanzisha muungano wa nchi tofauti kwa ajili ya kudhamini usalama wa kile kinachotajwa kuwa eti meli zinazopita katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, mpango ambao umekosa kuungwa mkono hata na waitifaki wa White House.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇