Licha ya kuwa sababu ya kushambuliwa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Aramco nchini Saudi Arabia inapasa kutafutwa katika vita vya Yemen lakini watawala wa Saudia na Marekani wanaelekeza sababu hiyo kwingine kwa kuituhumu Iran kuwa imehusika katika shambulio hilo.
Makelele ambayo yanapigwa na Marekani dhidi ya Iran kuhusiana na shambulio hilo yanalenga kuwatuliza watawala wa Riyadh ili ipate fursa ya kuendelea kuwakamua kifedha. Siasa za Marekani kuhusiana na Saudi Arabia zimesimama juu ya msingi wa kunufaika na dola za mafuta za nchi hiyo na jambo hilo bila shaka linadhaminiwa na kuendelea vita vya Yemen.
Safari ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekni huko Saidia na kuondoka nchini humo bila ya kujibu maswali ya waandishi wa habari akiwa na waziri mwenzake wa nchi hiyo ya kifalme, bila shaka ni jambo linalothibitisha kuwa haijakuwa rahisi kwa serikali ya Trump kumtuhumu kisiasa na kipropaganda muhusika bandia wa shambulio la Aramko.
Mapambano na hatua za kuzuia mashambulio ya adui, zinazotekelezwa na wananchi wa Yemen katika mazingira ya hivi sasa bila shaka haziwezi kulinganishwa na za mwanzo wa vita za mwaka 2015, ambapo sasa baada ya kupita karibu miaka mitano ya vita hivyo vya kichokozi, Wayemen wamevihamishia vita hivyo ndani ya mipaka ya Saudia yenyewe.
Wakati Yahya Saree', msemaji wa Jeshi la Yemen anaposema kwamba nchi hiyo kila siku inatengeneza droni 6 zilizo na teknolojia ya kisasa kabisa, suala hilo linabainisha wazi irada na hamasa kubwa ya wananchi wa Yemen katika kupambana na hujuma ya maadui ambapo sasa wamepata nguvu ya kuweza kushambulia vituo na viwanda muhimu zaidi vya Saudia kikiwemo cha Aramco.
Katika uwanja huo, Kamal Dehqani Firuozabadi, Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Kamati ya Usalama wa Kitaifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ameashiria ushujaa mkubwa ulioonyeshwa na watu wa Yemen katika kukilenga kiwanda cha mafuta cha Aramco na kusisitiza kwamba, operesheni hiyo imeidhalilisha Marekani licha ya kujigamba kuwa ina zana zote hizo za kijeshi, rada na makombora.
Katika mazingira hayo, ni wazi kuwa chanzo cha kushambuliwa kituo cha kusafisha mafuta cha Aramco kinafungamana moja kwa moja na mashambulio ya kichokozi yanayofanywa na muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia huko Yemen, na kuelekezwa tuhuma za shambulio hilo kwa upande wa tatu ni kutoamini uwezo mkubwa wa kijeshi wa taifa la Yemen.
Hali hiyo inathibitisha kwamba udhaifu wa kiulinzi wa Saidi Arabia umepelekea vituo vyake muhimu ndani ya ardhi ya nchi hiyo kulengwa na bila shaka chokochoko nyingine za Marekani katika eneo zitapanua zaidi nyufa za udhaifu huo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisema kuwa inafuatilia masuala ya kuimarisha amani na usalama wa Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na wala haiungi mkono vita, lakini kwamba iwapo mipaka yake itahujumiwa na adui, basi haitasita kuchukua hatua za kuilinda na kujitetea.
Kuhusiana na suala hilo, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mahojiano aliyofanya siku ya Alkhamisi na televisheni ya CNN ya nchini Marekani aliashiria matamshi ya kichochezi na ya kupenda vita yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa nchi hiyo dhidi ya Iran na kusema kuwa hakuna kile kinachotajwa na Wamarekani kuwa ni mashambulio madogo na ya muda mfupi. Alisisitiza kwamba Iran haitaki vita lakini haitasita kujitetea.
Iran imechukua hatua madhubuti za kulinda mipaka yake ya ardhini, baharini na angani na hatua yake ya hivi karibuni zaidi katika uwanja huo, ni kutungua droni ya kisasa kabisa ya Kimarekani katika Ghuba ya Uajemi. Nguvu ya Iran kumzuia adui kuanzisha hujuma ni ya ndani na wala haina uhusiano wowote na modola ya kigeni. Bila shaka jambo hilo linathibitisha wazi uwezo mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇