Rais Dkt. John Magufuli ametoa shilingi Milioni 10 kwa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu inayojiandaa kushiriki mashindano ya mpira wa miguu kwa watuwenyeulemavu Afrika (CANAF) yaliyopangwa kuanza tarehe 01Oktoba, 2019 katika Mji wa Benguela nchini Angola.
Katibu wa Rais, Ngusa Samike amekabidhi fedha hizo kwa viongozi na wachezaji wa timu hiyo leo tarehe 22 Septemba, 2019 katika studio za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambalo limekuwa likitangaza taarifa za timu hiyo kuomba msaada ili ifanikishe safari ya kwenda kushiriki katika mashindano hayo.
Samike amewasilisha ujumbe wa Rais Magufuli ambaye amewapongeza viongozi na wachezaji wa timu hiyo kwa dhamira yao ya kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo na amewatakia heri na ushindi.
Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wengine watakaoguswa kuisadia timu hiyo kufanya hivyo na kwatimu zingine zinazoiwakilisha Tanzania nje ya nchi kwa kuwa zinaitangaza Tanzania.
“Kwa watu wenye ulemavu kushiriki michezo pia ni tiba, kwahivyo nawapongeza kwa kushiriki michezo na mashindano haya naamini jamii itaendelea kutilia mkazo walemavu kushiriki michezo” amesema Samike.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu (TAFF) Peter Sarungi na Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu Hamad Komboza wamemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa msaada huo na kwa kuendelea kuwatambua na kuwathamani watu wenye ulemavu.
Wamesema timu hiyo yenye wachezaji 13, walimu 5 na viongozi 2 itaondoka tarehe 28 Septemba, 2019 kuelekea nchini Angola ambako inakwenda kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza na wameahidi kufanya vizuri.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC Matha Swai amemshukuru Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo wa kuchangia watu mbalimbali wenye uhitaji kila anapowaona kupitia vyombo vya habari na amehidi kuwa TBC itaendelea kutimiza jukumu lake la kuwatangaza watu hao ili watu mbalimbali wenye mapenzi mema wawaone na kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇