Na Said Mwishehe, Michuzi TV
HATIMAYE Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi Nape Nnauye(CCM) amejisalimisha kwa Rais Dk.John Magufuli kwa kwenda kumuomba msamaha kufuatia kuhusika kwake katika mazungumzo yasiyofaa dhidi ya Rais.
Siku za karibuni sauti ya Nape ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo sehemu ya mazungumzo yake yalisikika akitoa maneno ya kejeli kwa Rais Magufuli. Hivyo leo Septemba 10, 2019 amekutana na Rais kwa ajili ya kuomba msamaha.Wiki iliyopita Rais Magufuli atangaza kumsamehe Mbunge wa Jimbo la Bumbuli Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema William Ngeleja ambao nao sauti zao zilisikika wakimsema vibaya Rais.Wabunge hao walimuomba Rais msamaha na baada ya hapo Rais akatangaza kuwaseheme.
Taarifa iliyotolewa leo na Ikulu kwa vyombo vya habari imesema kuwa baada ya mazungumzo hayo Nape amemshukur Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kukutana nae na kumsikiliza, na pia kumsamehe kwa makosa aliyoyafanya kutokana na taharuki iliyoibuka baada ya kuvuja kwa sauti za mawasiliano yake na wanasiasa wengine wakimsema Rais Magufuli.
"Kwa hiyo baada ya kupata fursa nimekuja, nimemuona, na mle ambamo nilimkosea kama Baba yangu nimezungumza naye na Baba amenielewa.Ameniambia amenisamehe na amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo yatakwenda vizuri.
"Na kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua," amesema Nape.
Mbali ya kumuomba msamaha Rais Magufuli na kusamehewa,Nape ametumia nafasi hiyo kuzungumzia maendeleo yanayofanywa nchini kwetu, ambapo amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema ana matumaini kuwa CCM itapata ushindi katika chaguzi kutokana na kazi hiyo.
Kwa upande wake, Rais Magufuli amesema Nape amekuwa akiomba kukutana nae mara nyingi na tangu siku nyingi kupitia kwa watu mbalimbali wakiwemo wasaidizi wake, viongozi wastaafu na viongozi wa CCM, na baada ya kukutana nae na kumuomba radhi ameamua kumsahehe.
Rais Magufuli amemtaka Nape kwenda kufanya kazi za kuhudumia wananchi wa Jimbo lake la Mtama na kukitumikia vyema chama chake cha CCM."Yote nimesamehe, huyu bado ni kijana mdogo, ana matarajio makubwa katika maisha yake, mimi nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu na tumefundishwa katika maandiko yote tusamehe saba mara sabini.
"Kwa hiyo nimemsamehe na Mungu amsaidie katika shughuli zake akafanye kazi zake vizuri, akalee Mke wake na familia yake, akakitumikie chama, akawatumikie wananchi wa Jimbo lake vizuri, mimi nimemsamehe, labda kama yeye atakengeuka hiyo itakuwa ni juu yake,"amesema Rais Magufuli.
Pia ameongeza "Lakini mimi kutoka moyoni mwangu nimeshamsamehe na nimemsaheme kweli. Nape nenda ukafanye kazi, Mungu akujaalieee.
Nape alisikika akizungumza kwenye simu ambapo kwa sehemu kubwa mazungumzo yake yalina kumuomba msamaha baada ya sauti yake kusikika akimteta Rais kwenye simu ya mkononi siku za karibuni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuomba msamaha Rais Dkt. Magufuli kufuatia tukio lililotokea miezi iliyopita.
Mbunge wa Mtama Nape Nnauye akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mazungumzo yao pamoja na kusamehewa kosa aliliofanya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mbunge wa Mtama Nape Nnauye akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mazungumzo yao pamoja na kusamehewa kosa aliliofanya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mbunge wa Mtama Nape Nnauye akizungumza na Wanahabari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wanahabari mara baada ya mazungumzo yake na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇