Raia wa Zimbabwe watauaga mwili wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, hayati Robert Mugabe Alkhamisi ya leo.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Zimbabwe imesema kuwa, shughuli ya kuuaga mwili wa kiongozi huyo wa zamani wa taifa hilo, zitafanyika katika uwanja wa Rufaro, mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe. Uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu elfu 35, ni wenye historia ndefu, hasa kutokana na kuwa ndio uliotumiwa katika sherehe za kuapishwa mwanasiasa huyo mkongwe wa Zimbabwe hapo Aprili 1980 alipoingia madarakani nchini humo. Mugabe alifariki dunia tarehe 6 mwezi huu nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu ikiwa ni takribani miaka miwili tangu alipoondolewa madarakani.
Mwili wa Mugabe uliwasili Jumatano ya jana kwenye uwanja wa ndege wa Harare nchini humo ukitokea nchini Singapore. Viongozi na shakhsia mbalimbali wa nchi hiyo wakiongozwa na Rais, Emmerson Mnangagwa, familia na wananchi, walijitokeza uwanjani hapo kuupokea mwili wa mwanamapinduzi huyo aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 37. Baada ya mwili huo kuwasili Zimbabwe, ulipelekwa moja kwa moja nyumbani kwake. Habari zinasema kuwa, Rais Xi Jinping wa China, rais wa zamani wa Cuba, Raul Castrol na marais mbalimbali wa Afrika ni miongoni mwa watakaohudhuria mazishi ya hayati Robert Mugabe siku ya Jumamosi Septemba 14.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇