Baada ya kupita wiki kadhaa za uvumi wa vyombo vya habari kuhusiana na kuongezeka hitilafu za kimtazamo kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na mshauri wake wa usalama wa taifa, John Bolton, hatimaye Trump amechukua uamuzi wa kumfukuza mshauri wake huyo.
Akibainisha suala hilo kupitia ujumbe wa Twitter, Trump ameandika: 'Jana nilimfahamisha Bolton kwamba huduma yake haihitajiki tena White House. Mimi na maafisa wengine wa serikali tumekuwa tukipinga vikali mapendekezo yake mengi na ni kwa msingi huo ndipo nikamtaka awasilishe ombi lake la kujiuzulu naye akawa amefanya hivyo asubuhi. Ninamshukuru sana kwa huduma yake. Wiki ijayo nitamuarifisha mshauri mpya wa usalama wa taifa.'
Kwa uamuzi huo, mmoja wa maafisa wenye utata mkubwa na wachochezi wakubwa wa vita nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni amefutwa kazi White House. Bolton amekuwa mshauri wa tatu wa usalama wa taifa wa Marekani wa Rais Trump katika miaka miwili na nusu iliyopita. Tangu aingie White House, alitumia nguvu zake zote kufanya siasa za nje za Marekani ziwe dhidi ya mashiriki na taasisi za kimataifa na vilevile dhidi ya mataifa mengi ya dunia. Kumshawishi Trump aiondoe Marekani katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya maamuzi muhimu yenye utata yaliyochukuliwa na Bolton akiwa mshauri wa usalama wa taifa wa Trump. Kwa uamuzi huo si tu kwamba Marekani ilitengwa kisiasa katika ngazi za kimataifa bali hatua ya Iran kuamua kukabiliana na kusimama imara mbele ya mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani imevunja siasa za ubabe na za mabavu za serikali ya Trump.
Ni wazi kuwa uvurugaji wa Bolton wa siasa za nje za Marekani haukuishia tu katika suala la Iran na mapatano ya kimataifa ya JCPOA bali afisa huyo mwenye misimamo yenye utata mwingi katika miaka ya hivi karibuni alichukua hatua za uadui wa moja kwa moja dhidi ya mashirika na taasisi muhimu za kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa. Msimamo wake wa kibabe dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC uliwakera wengi duniani kiasi cha kuwafanya waseme kuwa uliashiria aina fulani ya kutangaza vita dhidi ya mfumo wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.
Bolton vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika kuwasha moto wa fitina na kuvuruga uhusiano wa Washington na Caracas ambapo aliipelekea Marekani kumtambua Juan Guaido kiongozi wa upinzani wa Venezuela kama rais wa nchi hiyo. Wakati huo huo, ushauri wake kuhusiana na Korea Kaskazini, China na Russia haukuwa na faida yoyote kwa Marekani.
Masuala hayo yote hatimaye yamemfanya Trump achukue uamuzi wa kumfukuza kazi Bolton ili kuzuia kuharibika zaidi siasa za nje na usalama wa Marekani.
Inasemekana kuwa suala la kualikwa kwa siri viongozi wa Taliban huko Camp David ambayo ni makao ya mapumziko ya msimu wa joto ya rais wa Marekani, ambalo karibuni limegeuka na kuwa kashfa kubwa ya kisiasa dhidi ya Trump, limekuwa risasi la mwisho lililommaliza Bolton.
Akizungumzia suala hilo, Kaitlan Collins, ripota wa CNN katika ikulu ya White House ameandika katika akaunti yake ya Twitter kwamba: 'Vyanzo viwili vya kuaminika vimeniambia kwamba jana usiku (Jumatatu usiku) Rais Trump na John Bolton, mshauri wake wa usalama wa taifa, waligombana vikali kuhusiana na kualikwa viongozi wa Taliban huko Camp David.'
Kwa vyovyote vile katika siku chache zijazo, Trump anapasa kumchagua mshauri wake wa nne wa usalama wa taifa. Tukiachilia mbali ni nani atakayeketi kwenye kiti cha Bolton, suala la kubadilishwa siasa za nje na za usalama za serikali ya Trump lina umuhimu mkubwa zaidi. Suala hilo linaweza kuwa na taathira kubwa katika siasa za ndani za Marekani na hasa katika kipindi hiki cha kukaribia kufanyika uchaguzi wa rais mwaka 2020 na vilevile kuwa na matokeo mazuri katika ngazi za kimataifa. Bila shaka jambo hilo litategemea moja kwa moja iwapo Trump mwenyewe anataka kujiweka mbali na zimwi la siasa haribifu za kivita za Bolton au la.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇