Ndugu wa karibu wa watu waliofariki kwenye ajali ya gari iliyotokea wilayani Kibiti mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kesho Jumatatu Septemba 2, kwaajili ya zoezi la kufanya uchunguzi wa kulinganisha Vinasaba (DNA) ili waweze kupewa miili hiyo.
Miili ya watu hao wanne wakiwa watu wazima na mmoja mtoto ilifikishwa katika hospitali hiyo jana Jumamosi asubuhi kwa ajili ya kuhifadhiwa ikiwa haitambuliki kutokana na kuharibika.
Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Septemba 1,2019 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MNH, Aminiel Aligaesha imesema miili hiyo imeungua kupita kiasi na kusababisha utambuzi wake kuwa mgumu.
“Jana saa tano asubuhi tumepokea miili ya marehemu watano wa ajali ya gari iliyotokea huko Kibiti ambapo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hivyo tunawaomba ndugu wa karibu wa marehemu waje kesho saa mbili asubuhi ili kuchukuliwa sampuli na Mkemia Mkuu wa Serikali ili kusaidia kufanya uchunguzi wa kulinganisha vinasaba kati ya ndugu na marehemu ili waweze kupewa miili hiyo kwa ajili ya mazishi baada ya uchunguzi kukamilika,” amesema.
Aligaesha amesema miili hiyo ambayo ni ya watu wazima wanne na mtoto mmoja imeungua sana hali iliyopelekea utambuzi wao kuwa mgumu lakini tayari wameshafanya uchunguzi na kuchukua sampuli kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali ili kufanya uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇