Baada ya kupita miezi kadhaa ya machafuko ya kisiasa nchini Sudan, hatimaye baraza jipya la mawazi la serikali ya mpito limetangazwa na hivyo kuchukuliwa hatua nyingine ya kivitendo ya kukabidhiwa madaraka kidemokrasia kutoka kwa wanajeshi.
Baada ya kupita wiki mbili tokea apishwe kuwa Waziri Mkuu mpya wa Sudan, Abdalla Hamdok ametangaza baraza lake la mawaziri. Akibainisha sababu ya kuchelewa kutangaza baraza hilo, Hamdok amesema kuwa imetokana na umuhimu wa kuwakilishwa Wasudan wote serikalini.
Kuchaguliwa waziri mkuu na kisha kubuniwa baraza la mawaziri kumetimia baada ya Baraza la Kijeshi na viongozi wa harakati ya upinzani kutiliana saini hati ya kikatiba tarehe 17 Agosti, iliyoandaa uwanja wa kutekelezwa takwa kuu la wapinzani, yaani kuundwa serikali ya kiraia ya mpito.
Kuafikiana juu ya hati hiyo ya kikatiba na kisha kutiwa saini wiki mbili baadaye, kumemaliza kivitendo machafuko ya kisiasa yaliyodumu nchini humo kwa muda wa miezi minane. Machafuko hayo yalifuatia malalamiko ya wananchi kuhusiana na siasa mbovu za kiuchumi za Rais Omar al-Bashir aliyeng'olewa madarakani na wanajeshi, na kuchukua sura mpya baada ya vyama vya siasa na wanaharakati wa demokrasia kujiunga na malalamiko hayo. Baada ya kushuhudia hali hiyo, wanajeshi waliamua kumpindua Jenerali Omar al-Bashir tareje 11 Aprili wakiwa na nia ya kutwa madaraka na kubuni baraza la kijeshi la mpito kwa ajili ya kuendesha mambo ya nchi.
Vitendo vya Baraza la Kijeshi na kufungamana kwa baadhi ya wanachama wake na utawala wa Sausi Arabia na vilevile hatua yake ya kuwaua Wasudan waliokuwa wamekusanyika nje ya makao ya jeshi tarehe 3 Juni ni mambo yaliyowakasirisha mno Wasudan na kuwafanya waendeleze harakati za kufuatilia malengo yao kuelekea demokrasia na kubuniwa serikali ya kiraia. Hatimaye Baraza la Kijeshi lilisalimu amri mbele ya mashinikizo ya wananchi na baadhi ya viongozi wa Kiafrika na wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutia saini hati ambayo ilitaka kubuniwa Baraza la Utawala, kuteuliwa waziri mkuu na kisha kubuniwa baraza la mawaziri kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu na kuboresha hali ya nchi hiyo.
Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Susan anasema: Tutafanya juhudi za kubuni serikali ya kidemiokrasia na kuheshimu tofauti zote za mitazamo. Vilevile tutabuni mipango ya kututua matatizo ya ughali wa maisha kwa kutilia maanani hali ya kiuchumi ya nchi, kudhamini mahitaji ya msingi na kuzingatia sekta ya uzalishaji.
Kuimarisha hali ya uchumi, usalama wa ndani na hasa katika maeneo kama vile Darfour, kutazama upya siasa za kigeni na kukomeshwa uingiliaji wa nje na hasa wa Saudia ni miongoni mwa matakwa muhimu ya watu wa Sudan.
Licha ya kuwa hatua nyingine muhimu imepigwa katika uwanja wa siasa za Sudan lakini bado wengi wana wasiwasi kuwa changamoto kama vile za kuongezeka uingiliaji wa wanajeshi na juhudi zao za kusalia serikalini, huenda zikavuruga mkondo wa matakwa ya kidemokrasia ya wananchi wa nchi hiyo. Historia ya Sudan pia inaonyesha wazi kuwa katika umri wa miaka 63 ya uhuru wa nchi hiyo tokea mwaka 1956 hadi sasa, wanajeshi na vibaraka wao wamekuwa wakitawala nchi hiyo, hivyo kuimarisha demokrasia na juhudi za kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki halitakuwa jambo rahisi katika uhai wa kisiasa wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Abdulfattah al-Burhan, mkuu wa Baraza la Kijeshi lililovunjwa la Sudan anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Mapinduzi ya Sudan yamefikia malengo yake kupitia juhudi za wananchi na sasa tunahitaji kupiga hatua kuelekea mustakbali ili tuifanye leo yetu kuwa kituo cha kusahau machungu yetu yaliyopita.
Inaonekana kuwa matukio ya Sudan yameingia katika hatua ya kubaleghe, na iwapo jambo lolote lisilotarajiwa halitatokea, Sudan katika miaka ya usoni na kupitia ushirikiano wa watu wake, inaweza kubadilika na kuwa moja ya nchi za kupigiwa mifano mizuri ya demokrasia barani Afrika. Jambo hilo bila shaka lina umuhimu maalumu kwa kutilia maanani nafasi ya ukubwa, eneo la kijografia, utajiri na historia ya kisiasa ya nchi hiyo kubwa ya Kiislamu barani Afrika.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇