Kongamano la biashara la Uganda na Tanzania limefanyiika leo jijini Dar es Salaam huku suala la ujenzi wa bomba la mafuta baina ya nchi mbili likitawala mkutano huo.
Akihutubia katika kongamano hilo, Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemtaka mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni kuwa mkali kwa watendaji wake ambao wanakwamisha kuanza mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Tanga Tanzania.
Rais Magufuli amesema kuwa, Serikali yake ilifanya mabadiliko ya sheria ili kupunguza sehemu ya kodi kwa ajili ya mradi huo. Rais wa Tanzania amemtaka Rais Museveni wa Uganda kuchukua hatua kali nchini kwake kwa kuwa tayari kupoteza kidogo kama Tanzania ilivyofanya iili ipate kikubwa zaidi.
Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemshauri Rais huyo wa Uganda akimwambia kwamba, kama washauri wake ndiyo kikwazo basi asisite kuwaondoa na kuwaweka wengine.
Kadhalika Rais John Pombe Magufuli amewataka watendaji katika nchi za Uganda na Tanzania wahakikishe wanafanikisha miradi mikubwa ambayo inatengeneza ajira nyingi.
Kwa upande wake Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amemhakikishia Rais wa Tanzania kwamba, serikali yake itahakikisha bomba hilo la mafuta linajengwa na mafuta ambayo yamekuwepo kwa miaka mingi yanapatikana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇