Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali jinai mpya zilizofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia huko nchini Yemen.
Sayyid Abbas Mousavi amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani shambulio la anga lililofanywa na Saudi Arabia dhidi ya jela ya Al Maqsuf katika mji wa Dhamar huko nchini Yemen na kupelekea makumi ya wafungwa kuuawa.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonyesha kusikitishwa mno na jinai hizo mpya za Saudi Arabia na kueleza kwamba, jinai hizo zinafanyika kwa kutumia silaha za Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi.
Zaidi ya watu sabini wameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Saudi Arabia dhidi ya jela ya Al Maqsuf, huku operesheni za utoaji misaada na kufukua maiti na majeruhi waliokwama kwenye vifusi zikiwa zinaendelea.
Alfajiri ya kuamkia leo, mkuu wa amati ya taifa ya kushughulikia mateka wa Yemen Abdulkadir Al-Murtadha alitangaza kuwa, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umeshambulia kwa makombora jela ya Al Maqsuf iliyoko mkoani Dhamar.
Tangu Machi 2015 na baada ya kupita zaidi ya miaka minne ya mauaji ya maelfu kwa maelfu ya raia sambamba na kuteketeza miundombinu ya Yemen, Saudi Arabia na waitifaki wake hadi sasa wameshindwa kufikia malengo yao katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu kutokana na muqawama wa wananchi wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇