Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye jana aliwasili nchini India pamoja na mkewe kwa ajili ya matibabu, huenda akalazimika kuondoka nchini humo kutokana na mazingira yasiyofaa ya matibabu.
Ripoti kutoka India zinasema kuwa, Sheikh Zakkzaky amekuwa akitibiwa katika mazingira ya usimamizi mkali wa usalama hali ambayo amesema ina taathira hasi kwa mwenendo wa matibabu yake nchini humo.
Baadhi ya duru zilizoko karibu na Sheikh Zakzaky zinasema kuwa, huenda mwanazuoni huyo pamoja na mkewe wakalazimika kuondoka nchini India na kurejea Nigeria kwani, mashinikizo na usimamizi mkali wa usalama umekuwa ukikwamisha mwenendo wa matibabu yake.
Aidha ripoti nyingine zinasisitiza kuwa, hata madaktari wanaomtibu Sheikh Zakzaky walikwishaanishwa tangu hapo kabla hali inayoonyesha kwamba, maafisa usalama wa Nigeria wanahusika moja kwa moja katika mchakato mzima wa kuainisha madaktari na hata hospitali aliyopokewa Sheikh Zakzaky.
Baada ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe kuwasili India, ubalozi wa Nigeria nchini humo jana ulitoa taarifa na kutangaza kuwa mwanazuoni huyo yuko chini ya udhibiti wa ubalozi huo.
Kwa mujibu wa mawakili wanaomtetea kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, jicho la kulia la Sheikh Zakzaky limepoteza nguvu za kuona na kuna uwezekano jicho lake jingine pia likapata tatizo kama hilo. Mazingira anayokabiliwa nayo Sheikh Zakzaky huko India yameanza kuwatia wasiwasi wafuasi wa mwanaharakati huyo juu ya mustakabali wa afya yake.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇