Hatua ya serikali ya India ya kuweka vizuizi na kubana shughuli za kidini katika eneo la Kashmir imekabiliwa na radiamali kali ya Pakistan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetangaza kupitia taarifa iliyotoa kwamba vizuizi na mbinyo uliowekwa na India katika eneo la Kashmir umewafanya maelfu ya Waslamu wa eneo hilo washindwe kushiriki kwenye Swala ya Idul Adh'ha na marasimu mengine ya kidini. Taarifa hiyo imeongeza kuwa kuwazuia watu kutokuwa na uhuru wa kidini ni kinyume na sheria za kimataifa na ni ukiukaji wa waziwazi wa kanuni za haki za binadamu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imeitolea wito jamii ya kimataifa khususan Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kupinga hatua hizo za India za kuwanyima Waislamu wa Kashmir uhuru wa kidini. Mbinyo huo mkali wa kidini unatekelezwa kwa Waislamu wa eneo la Kashmir katika hali ambayo siku kadhaa zilizopita serikali ya India ilifuta kipengee cha 370 cha katiba ya nchi hiyo na hivyo kuliondolea mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir. Hasa ikitiliwa maanani kuwa masaa kadhaa baada ya kutangazwa kufutwa mamlaka ya kujitawala eneo hilo; chama tawala India cha Bharatiya Janata (BJP) kilituma haraka makumi ya maelfu ya wanajeshi huko Kashmir na kisha kikakata huduma za intaneti na simu na kuwatia nguvuni wakuu wa makundi ya Kikashmiri.
Hatua ya serikali ya India ya kulifutia eneo la Kashmir mamlaka ya kujitawala licha ya kupingwa ndani ya nchi hiyo; kukiwemo kupingwa na chama cha Kongresi ambacho kimeitaja hatua hiyo kuwa ni maafa, vile vile imepingwa na baadhi ya nchi duniani.
Hata hivyo Radiamali ya Pakistan imekuwa kali sana ikilinganishwa na ya nchi nyingine; ambapo nchi hiyo imeamua kumfukuza balozi na wanadiplomasia wa India huko Islamabad na kukata uhusiano wake wa kibiashara na India. Serikali ya India imejibu hatua hizo za Pakistan ikisema kuwa uamuzi iliochukua hivi karibuni kuhusu eneo la Kashmir, ni kadhia ya ndani na kuitaka Islamabad kutazama upya uamuzi wake huo wa kupunguza uhusiano kati yake na New Delhi.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ya kulalamikia mbinyo na vizuizi vya kidini vilivyowekwa na serikali ya India katika eneo la Kashmir inaonyesha kuwa ule utabiri kuhusu kufutwa mamlaka ya kujtawala eneo hilo kukiwemo kushadidishwa mbinyo na vizingiti mbalimbali dhidi ya Waislamu wa Kashmir ulikuwa sahihi; na lengo la chama tawala la BJP ni kuzidisha mashinikizo dhidi ya Wakashmiri na kuwalazimisha kuondoka katika eneo hilo.
Serikali ya India inaonekana kushadidisha zaidi vitendo vya kuwabinya na kuwabana raia wa Kiislamu wa Kashmir kuliko huko nyuma kwa kulifutia eneo hilo mamlaya yake ya kujitawala; hatua ambayo inaweza pia kuchochea zaidi moto wa machafuko katika eneo hilo. Serikali ya India inatekeleza siasa sawa kabisa na zile za serikali ya Myanmar kwa kuzidisha vitendo vya mabavu na ukandamizaji dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo ambapo jamii hiyo ya Waislamu imelazimika kuyaacha makazi yake na kuelekea katika maeneo ya mpakani nchini Bangladesh. Serikali ya India inawawekea vizuizi na mbinyo wa kidini Waislamu wa Kashmir ili kuwalazimisha kuondoka katika eneo hilo na kuelekea upande wa Pakistan na katika nchi nyingine jirani.
Ni katika fremu ya stratejia hii ambapo serikali ya India katika hatua yake ya awali kabisa baada ya kulifutia eneo la Kashmir mamlaka ya kujitawala ikaamua kuanzisha duru mpya ya mashinikizo dhidi ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwawekea vizuizi na vizingiti katika kutekeleza shughuli zao za kidini kukiwemo kuwazuia kuswali Swala ya Idul -Adh'ha.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇