LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 11, 2019

RAIS MAGUFULI: TUWAOMBEE MAJERUHI, WALIOPOTEZA MAISHA, TUSIWE WEPESI KUHUKUMU


Rais Dkt. John Magufuli amewatembelea na kuwapa pole majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambao wameungua moto katika ajali iliyotokea jana asubuhi Mjini Morogoro baada ya mafuta yaliyokuwa yakimwagika kutoka kwenye lori lililopinduka kulipuka moto.

Ajali hiyo imesababishavifo vya watu 71 mpaka sasa.
Majeruhi 46 wamefikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa magari ya wagonjwa na helkopta na majeruhi wengine wanaendelea kupatiwa matibabu Mkoani Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru na Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa wa Dharura cha hospitali hiyo Dkt. Juma Mfinanga wamemueleza Rais Magufuli kuwa wagonjwa 46 waliofikishwa hospitalini haponi wale walioungua kwa kiwango kikubwa cha hadi takribani asilimia 100 na kwamba wa 3 kati yao wamefariki dunia baada ya kufika.

Pamoja na kuwapa pole,  Rais Magufuli amewataka Watanzania kutokuwa wepesi wa kuwahukumu kwa madai walikuwa wakiiba mafuta, kwani baadhi yao walikwenda eneo la tukio kwa lengo la kutoa msaada, wengine walikutwa na moto wakiwa katika maeneo yao ya kazi na wengine walikutwa na moto wakiwa wanasafiri katika magari yao.

Rais Magufuli amewashukuru Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Jeshi la Ulinzi la Wananchiwa Tanzania (JWTZ) kwa juhudi kubwa wanazozifanya kutoa matibabu kwa majeruhi hao na ameagiza kuwa gharama za matibabu na huduma nyingine kwa majeruhi hao zitatolewa na Serikali.

“Nawashukuru sana Madaktari na Manesi, wanafanya kazi kubwa sana, kweli wanafanya kazi kubwa sana, nimewaona wagonjwa wanahudumiwa vizuri, lakini kikubwa sisi Watanzania tumtangulize Mungu mbele, tuwaombee hawa wagonjwa, lakini na wale waliotangulia mbele za haki nao tuwaombee, naniwaombe ndugu zangu Watanzania katika ajali tusiwe wepesi wa kuhukumu, nimefika humu wodini nimemkuta mmoja ni dereva wa lori la mafuta, alipofika pale aliamua kushuka aende akasaidie, lakini nae ameungua na amelazwa hapa, yupo mwingine alikuwa anasafiri kwenda Mtwara, wala hakwenda kuchukua mafuta, nae ameungua” amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na wananchi waliokuwa nje ya wodi ya Kibasila.

Aidha, Rais Magufuli ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwatangaza majeruhi wote kwa majina yao na mahali wanakotoka ili ndugu na jamaa zao wapate taarifa.

Katika hatua nyingine,  Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museruku mruhusu Rahel Kitwai Roita mkazi wa Turiani Morogoro kuuchukua mwili wa Marehemu mama yake, baada ya mwili huo kuzuiwa kutokana na kudaiwa zaidi ya shilingi Milioni 5 ambazo ni gharama za matibabu.Rahel Kitwai Roita ametoa ombi hilo akiwa pembezoni mwa njia ya kupita wagonjwa ambapo  Rais Magufuli ametaka deni hilo la shilingi Milioni 5 adaiwe yeye na ametoa rambirambi ya shilingi laki 5.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages